Jukwaa
la Wakristo Tanzania (TCF) limetoa tamko kuhusiana na hali ilivyo sasa
Zanzibar likisema linafadhaishwa na kusikitishwa nayo na kwamba
linaamini isingefikia hapo endapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ingechukua hatua katika kutatua mgogoro huo.
Katika
tamko hilo lililosambazwa kwenye vyombo vya habari jana baada ya kikao
cha TCF juzi, yamo mapendekezo manne likiwamo la kuitaka Serikali
kurejesha mchakato wa Katiba kwa kuzingatia maudhui yaliyomo katika
Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ili kuondoa utata wa Serikali
kushiriki masuala ya Zanzibar.
“Sisi viongozi wa dini tuliokutana leo tarehe 15.03.2016, tunafadhaishwa na kusikitishwa na hali ya Zanzibar kwa sasa.
"Hali
ya Zanzibar isingefika hapo ilipo iwapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ingechukua hatua ya kutatua mgogoro huu.
"Hali
hii ya Zanzibar na udhaifu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano vinapelekea
kushindwa kwa Serikali ya Muungano kuchukua hatua ya kusaidia hali ya
Zanzibar. Hata hivyo, udhaifu huu wa Katiba hauondoi wajibu wa Serikali
ya Muungano kuhakikisha haki na amani vinatawala Zanzibar,” ilisema sehemu ta tamko hilo lililotiwa saini na Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Mwanza, Jude Ruwa’ichi.
Jukwaa
halikufafanua hali ya Zanzibar kwa sasa inay- osababisha maaskofu hao
kufadhaika lakini huenda limekusudia kueleza hofu iliyotanda katika
visiwa hivyo tangu Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilipofuta uchaguzi na
matokeo yote ya uchaguzi wa Zanzibar, na baadaye kutangaza kuwa
utarudiwa Machi 20.
Vyama tisa kikiwamo Chama cha Wananchi (CUF) vilitangaza kujitoa lakini ZEC imesisitiza vyama vyote vitashiriki.
Hali
imeendelea kuwa tete na hivi karibuni yamekuwapo matukio ya uchomaji
moto makazi ya watu katika visiwa hivyo yanayoonyesha uvunjifu wa amani
kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa marudio Jumapili ijayo.
Baadhi
ya matukio hayo ni kuchomwa moto maskani za CCM na CUF, nyumba 11 za
watu ikiwamo ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame iliyoko
Kijichi, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Baada
ya kutathimini hali hiyo, TCF imesema pamoja na udhaifu wa Katiba,
Serikali ya Muungano bado ina wajibu wa kuhakikisha uhuru, haki na amani
vinatawala Zanzibar kuelekea uchaguzi huo wa marudio.
“Hata
hivyo, Serikali ya Muungano pamoja na taasisi zinazosimamia mchakato wa
uchaguzi, zinao wajibu wa kuhakikisha kuwa suala la uhuru, haki na
amani Zanzibar vinalindwa na kuheshimiwa. Suala la uhuru, haki ni wajibu
wetu sisi viongozi wa dini na Watanzania wote na halina mbadala,” ilisema sehemu ya tamko hilo.
Jukwaa
limesisitiza kwamba ni jukumu la kila mmoja kutimiza wajibu wake
kulinda uhuru, haki na amani na kuweka uzalendo kwanza kuliko
kutanguliza maslahi binafsi au ya vyama vya siasa.
Mbali
ya pendekezo la kuitaka Serikali kurejesha mchakato wa Katiba, pia
limewataka viongozi wa dini kuwahimiza Watanzania wote kuendelea
kuiombea Tanzania (Bara na Zanzibar) ibaki kuwa Taifa lililojengwa
katika msingi ya uhuru, haki na amani.
Pili,
limelitaka Jeshi la Polisi, vikosi vya ulinzi na usalama na Jeshi la
Wananchi wa Tanzania, kwa wakati huu kuendelea kutimiza wajibu wa
kusimamia amani na taratibu kwa haki bila upendeleo.
Mwisho
limesisitiza kwamba viongozi wa dini wabaki kuwa sauti ya kinabii na
wahubiri wa uhuru, haki na amani wakati huu, wakati wa uchaguzi na haada
ya uchaguzi.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )