MKURUGENZI
Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Wilaya ya Maswa
(MAUWASA) mkoa wa Simiyu, Lema Jeremiah (50) amefikishwa katika Mahakama
ya Wilaya ya Maswa akikabiliwa na makosa ya wizi wa Sh milioni 108 mali
ya serikali.
Mwendesha
Mashitaka wa Polisi, Nassib Swedy alidai mbele ya Hakimu Mkazi wa
mahakama hiyo, Tumaini Marwa kuwa mshitakiwa anatuhumiwa kufanya wizi wa
fedha akiwa mtumishi wa Umma.
Swedy
alidai Machi 7 mwaka 2014 saa 3:00 asubuhi, Jeremiah akiwa katika Ofisi
za Mamlaka hiyo zilizoko katika kijiji cha Sola wilayani humo aliiba Sh
milioni 108 zikiwa ni mali ya Serikali zilizotolewa na Mwajiri wake
ambaye ni Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Alisema kosa hilo ni kinyume na Kifungu cha 270 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.
Hata
hivyo, mara baada ya kusomewa shitaka hilo mshitakiwa huyo alipoulizwa
na hakimu Marwa kuhusika nalo, alikana kosa hilo na mwendesha mashitaka
kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe
nyingine ili waendelee na upelelezi na kesi hiyo itatajwa tena Aprili 11
mwaka huu.
Hakimu
Marwa alisema masharti ya dhamana kwa mshitakiwa anatakiwa awe na
wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh milioni 50 au hati ya mali
isiyohamishika yenye thamani ya Sh milioni 50 na hati hiyo itatakiwa
ikaguliwe kama kweli inafikia kiasi hicho.
Mshitakiwa
amekidhi vigezo hivyo na kuachiwa kwa dhamana, lakini alipotoka
mahakamani akashikiliwa na Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) kwa madai kuwa anahitajika kwa mahojiano zaidi
kutokana na tuhuma nyingine zinazomkabili.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )