Featured
Loading...

Rais John Magufuli Katikati ya Kagame, Museveni na Kenyatta


Wakati Rais Paul Kagame wa Rwanda akiiga staili ya kupiga marufuku safari za nje, Uhuru Kenyatta wa Kenya atakuwa akijutia uamuzi wa Rais Yoweri Museveni wa Uganda pamoja na John Magufuli kuhamishia Tanzania mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi.

Akizungumza katika mkutano wa kutathmini utendaji wa viongozi, Rais Kagame alisema anakubaliana na Rais Magufuli kudhibiti safari za nje kwa sababu zinapoteza muda na rasilimali za nchi.

Wakati Kagame akisema hayo Jumamosi, Museveni alikubaliana na Rais Magufuli kujenga bomba la mafuta ghafi kutoka Tanga hadi Uganda kujiandaa kusafirisha mafuta hayo ambayo yanatarajiwa kuanza kuvunwa kwenye nchi hiyo jirani mwaka 2018.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana, mradi huo mkubwa utaanzia Ziwa Albert nchini Uganda kuishia Bandari ya Tanga, badala ya mradi wa awali ambao ulitakiwa kujengwa hadi Bandari ya Lamu nchini Kenya.

Agosti mwaka jana, Kenya na Uganda zilitia saini makubaliano ya ujenzi wa bomba hilo. Hata hivyo, wataalamu kutoka kampuni ya Total ya Afrika Mashariki walisisitiza kwamba Tanzania ndiyo njia nzuri na salama na itakayopunguza gharama za ujenzi wa bomba hilo.

Uganda ilikuwa ikitazamia kutumia njia mbadala ambazo ni ile ya kutoka Hoima – Lacor – Lamu, Hoima – Nairobi – Mombasa na sasa Hoima – Tanga. Hata hivyo, njia ya Lamu iliyoko kaskazini mwa Kenya ilionekana kuwa na tishio la kiusalama kutoka kundi la kigaidi la Al Shabab.

Kadhalika, waliogopa kupitisha bomba hilo katikati ya jiji la Nairobi kwa sababu miundombinu mingi ingebomolewa. Wataalamu hao wamependekeza kupitisha bomba hilo katika bandari ya Tanga kwa sababu ni salama, gharama zake si kubwa kutokana na ufupi.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Serikali ya awamu ya nne kulalamikiwa kwa kuchelewa kufanya uamuzi na kusababisha Tanzania kutengwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo na muungano wa baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki zilizojiita Umoja wa Walio Tayari.

Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total Afrika Mashariki, Javier Rielo jana alimtembelea Rais John Pombe Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam na kumhakikishia kuwa kampuni hiyo itaanza ujenzi wa mradi huo haraka iwezekanavyo, kwa kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zipo.

Bomba hilo ambalo litakuwa na uwezo wa kusafirisha mafuta ghafi kiwango cha mapipa 200,000 kwa siku na linatarajiwa kuzalisha ajira 1,500 za moja kwa moja na ajira nyingine 20,000 zisizo za moja kwa moja.

Rielo alisema bomba hilo litagharimu dola 4 bilioni za Marekani (Sh8.7 trilioni).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu, Rais Magufuli ameitaka kampuni hiyo kuharakisha mchakato wa kuanza kwa mradi, na ameshauri muda wa miaka mitatu uliopangwa kuukamilisha mradi huo upunguzwe, ili manufaa yake yaanze kupatikana mapema.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema wizara yake ipo tayari kuhakikisha mradi huo unafanikiwa, na itatoa ushirikiano wa kutosha kuharakisha utekelezaji wake.

Alisema Tanzania inatarajia kunufaika na bomba hilo kwa kuwa kuna tafiti mbili za mafuta zinazoendelea katika ziwa Tanganyika na ziwa Eyasi, ambazo zikikamilika kwa mafanikio inatarajiwa bomba hilo litasaidia kusafirisha mafuta yake.

Naye  Rais wa Rwanda Paul Kagame amepiga marufuku safari za nje kwa mawaziri  mpaka kwa kibali maalum ili kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali.

Paul Kagame alilaumu Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kutumia pesa ‘kiholela’ kutokana na mawaziri kufanya ziara za mara kwa mara kuhudhuria mikutano.

Alisema mawaziri wa nchi yake wanatumia chombo hicho kama njia ya kujinufaisha kwa kufanya ziara na kuhudhuria mikutano ya jumuiya hiyo isiyo muhimu.

Aliahidi kuiga mfano wa Rais wa Tanzania John  Magufuli kutokomeza ufisadi huo wa kusitisha ziara za mawaziri alizotaja kuwa za kufuja mali ya taifa.

Akiongea katika mkutano wa faragha wa viongozi wa taasisi zote za Serikali nchini Rwanda, Rais Kagame alisema suala la ufisadi nchini humo linachukua mwelekeo mpya na kasi ya ajabu na kwamba hawezi kuendelea kuvumilia.

“Mawaziri wetu sasa wana kazi za ushauri kwa nchi nyingine kuliko wanavyofanya kazi za ndani ya nchi yao, Magufuli aliwazuia na mimi nawazuia ’’alisema

Kagame aliahidi  kupunguza gharama kwa safari ambazo hazina umuhimu za  mikutano ya EAC kwani viongozi wengi wanasafiri wakati kuna waziri husika anayeweza kwenda mwenyewe na kuwakilisha nchi.

“Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Valentine Rugwabiza, pekee anaweza kusafiri kama mjumbe, hivyo ikiwa kuna  hata waziri anataka kwenda kwenye mkutano huo awasiliane na waziri huyo na ndiye atakayekuruhusu ikiwa kuna ulazima,’’ alisema

Alisema  mawaziri wake wasiopungua watano wanasafiri zaidi ya  mara tatu kwa wiki kushiriki mikutano ya EAC popote inapotokea katika nchi wanachama na kwamba ziara hizo zinaigharimu Serikali kiasi kikubwa cha fedha.

“Ni kama mawaziri wa nchi hizi walikubaliana kushinikiza Serikali zao kuwa lazima wahudhurie kila aina ya vikao vya jumuia hii kwa kisingizio kuwa waziri anayeshindwa kuhudhuria nchi yake inachukuliwa hatua ama inaonekana kupinga juhudi na mikakati ya jumuiya,” alisema Rais Kagame.

Moja ya njia alizosema anaweza kutumia ni kumpa waziri wake wa masuala ya EAC Valentine Rugwabiza jukumu la kushughulikia masuala yote yanayohusu jumuiya hiyo

Alipongeza juhudi za Magufuli za kukomesha  ufisadi uliokuwa umekithiri katika taasisi za Serikali, akisema lazima na yeye afuate nyayo zake katika suala zima la kukomesha ufisadi na ufujaji wa mali ya Serikali.

Kagame aliyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa umma zaidi ya 250  kuhusu mipango ya nchi yake ya mwaka 2020 na kuahidi kubana matumizi serikalini ili kusaidia kukuza uchumi wa nchi hiyo.

Machi 2, Mwenyekiti mpya wa EAC, Rais Magufuli aliwashangaza wakuu wenzake wa jumuiya hiyo baada ya kuponda gharama kubwa zilizotumika kuandaa mkutano wa 17 wa wakuu hao, akisema zingeweza kuokolewa na kufanya kazi nyingine kwa gharama nafuu.

Dk Magufuli aliitaka sekretarieti  ya jumuiya hiyo kubana matumizi kwa kuwa inaongoza watu walio masikini.

Alisema mkutano kama huo ungeweza kufanyika sehemu nyingine kwa gharama nafuu.

Alieleza kushangazwa kwake kuona umetumia gharama kubwa kwa kila mjumbe kulipiwa dola 45 za Marekani kiasi ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na ukumbi wa AICC.

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top