Uongozi
mkoani Mbeya umeifunga Shule ya Sekondari Iyunga baada ya mabweni
matatu kuungua moto na wanafunzi kulala nje kutokana na kuyaogopa
mabweni yaliyobaki.
Kwa
kawaida likizo fupi ilitakiwa kuwa kipindi cha pasaka, lakini shule
hiyo ilifungwa Machi 11 hadi 25 na kwamba itaendelea kufungwa hadi
Aprili Mosi.
Mkuu
wa shule hiyo, Edward Mwantimwa alitoa maelezo hayo kwa Naibu Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jaffo aliyefika shuleni hapo
juzi kujionea uharibifu uliotokana na moto uliounguza mabweni matatu kwa
nyakati mbili tofauti.
Mwantimwa
alisema mara ya kwanza mabweni ya Nyerere na Mkwawa yaliungua Februari
29 na Machi 7 la Shaban Robert, jambo ambalo lilisababisha hofu kwa
walimu na wanafunzi na kuanza kuyasusa mabweni mengine.
Awali,
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Nyirembe Munasa akizungumza kwa niaba ya mkuu
wa mkoa alimueleza naibu waziri hatua zilizochukuliwa ikiwamo wadau
kutoa misaada na kwamba, pia walikuwa wanaandaa harambee ambayo
wangependa ifanyike Dar es Saalaam.
Jaffo alilitaja tukio hilo kuwa ni janga na kuahidi kuwashirikisha wabunge wote kuchangia kurudisha hadhi ya shule hiyo.
“Kuungua kwa shule hii kumeonyesha mengi yakiwamo ya uchakavu wa miundombinu,” alisema.
Alimtaka Nyirembe kusimamia ukarabati wa shule hiyo na uwe umekamilika ifikapo Aprili Mosi.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )