Maafisa
wa Takukuru na askari wa Jeshi la Polisi waliokuwa wakilinda eneo la
Mahakama ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, juzi nusura watwangane
makonde wakati wakimgombea shahidi.
Tukio
hilo lilianza kama masihara baada ya shahidi huyo kufika mahakamani
akiongozana na maofisa wa Takukuru na ghafla mmoja wa polisi
aliyemtambua, alimuweka chini ya ulinzi na kumfunga pingu.
Kamanda
wa Takukuru wa wilaya hiyo, Chuzela Shija alilazimika kuingilia kati na
kuwaomba polisi kumuachia mtu huyo, Paulo Sitephano ili atoe kwanza
ushahidi ndipo hatua nyingine zifuate, ombi lililokubaliwa na polisi kwa
kumfungua pingu huku wakimlinda asitoroke.
Sokomoko
lilianza mara tu shahidi huyo alipomaliza kutoa ushahidi dhidi ya
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Umoja anayetuhumiwa kuomba na kupokea
rushwa ya Sh100, 000.
Polisi
hao walimuwahi na kumfunga tena ili wampeleke kituoni. Kitendo hicho
kiliwakera maofisa wa Takukuru ambao walitaka kuondoka na mashahidi wao
wote watano walioenda nao mahakamani hapo kwa kutumia gari lao.
Maofisa
hao wa Takukuru waliwasihi polisi kumuacha shahidi huyo na kuwataka
wamkamate baada ya kukamilisha taratibu zao za kiofisi, ombi hilo
lilikataliwa na askari hao.
“Hatuwezi kumuachia mtuhumiwa kwa sababu anatafutwa muda mrefu kwa tuhuma zilizofikishwa polisi,” alijibu mmoja wa polisi aliyekuwa na cheo cha sajenti ambaye alikataa kutaja jina lake.
Kitendo
hicho kiliwakera maofisa wa Takukuru na kuamua kutumia nguvu kuwazuia
polisi kuondoka na shahidi wao, hali iliyozua mtafaruku baina yao na
kufikia hatua ya kukunjana mashati kabla ya kuamuliwa kuacha vitendo
hivyo.
Baada
ya vuta nikuvute na kurushiana maneno makali na vitisho, polisi
walioongeza nguvu kwa kuita gari la doria, walifanikiwa kumchukua
shahidi huyo na kumpandisha kwenye gari kabla ya kuondoka naye, huku
maofisa wa Takukuru wakibaki kulalamikia ubabe wa askari hao.
Katika
tukio hilo lililovuta watu wengi, baadhi ya maofisa wa Takukuru
walionekana wana nguo zilizochanika, hali iliyosababishwa na mtafaruku
huo.
Akizungumzia
tukio hilo, mkuu wa waendesha mashtaka wa polisi mahakamani hapo, Elias
Mgobela aliwatupia lawama maofisa wa Takukuru kwa kushindwa kuonyesha
ushirikiano kwa askari hao wakati wa kumtia mbaroni mtuhumiwa.
“Kisheria,
polisi wana haki ya kumkamata mtuhumiwa eneo lolote. Huyo shahidi wa
Takukuru alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu na polisi. Ilikuwa ni jukumu
la maofisa wa Takukuru kushirikiana na polisi kufanikisha kumkamata
badala ya kuzuia,” alisema.
Alisema
kitendo hicho kilisababisha mmoja wa watuhumiwa aliyemtaja kwa jina
moja la Lubango aliyekuwa chini ya ulinzi wa polisi kutoroka baada ya
askari wengi kuelekeza nguvu kumgombea shahidi huyo.
Kwa
upande wake, kamanda wa Takukuru wa wilaya, Chuzela Shija aliitupia
lawama polisi akidai ilitumia ubabe, nguvu na dharau dhidi ya maofisa
wake ambao hawakukataa shahidi wao kutiwa mbaroni, bali waliomba wapewe
fursa ya kukamilisha taratibu za kiofisi kabla ya kumkabidhi mikononi
mwao kwa tuhuma zinazomkabili.
“Isingewagharimu
polisi kufuatana na maofisa wa Takukuru hadi ofisini, wakakamilisha
taratibu za kiofisi na shahidi huyo, halafu wakamtia mbaroni.
Ilihitajika busara ndogo sana kulimaliza suala hili, lakini bahati mbaya
wenzetu walichagua kutumia ubabe na kutunishiana misuli,”alilalamika.
Katika
kesi dhidi ya mwalimu huyo, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Amani Mwenegoha
aliieleza mahakama jinsi alivyoshiriki kuweka mtego wa kumnasa.
Mkuu
huyo wa wilaya alidai kuwa aliandaa mtego huo na kufanikiwa kumtia
mbaroni mtuhumiwa huyo, Daniel Nying’ati baada ya kupokea malalamiko
kutoka kwa mmoja wa wananchi aliyedai kuombwa fedha ili mtoto wake apate
nafasi ya kurudia darasa la saba shuleni hapo.
Akiongozwa
na mwendesha mashtaka wa Takukuru, Kelvin Murusuri, shahidi huyo alidai
kuwa alichukua jukumu hilo kutekeleza moja ya majukumu yake ya kupokea,
kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Alidai
Februari 8, alipokea simu kutoka kwa mwananchi aliyemtaja kwa jina la
Marko Elias akimtaarifu kuombwa rushwa na mwalimu Mkuu wa Shule ya
Msingi Umoja alipoenda kuomba nafasi ya mtoto wake kurudia darasa la
saba shuleni hapo.
“Katika
maelezo yake, mwananchi yule aliniambia aliombwa rushwa ya Sh150, 000,
ndipo nilipomuambia aende Takukuru na kufanikisha mtuhumiwa kutiwa
mbaroni,” alidai Mwenegoha.
Kwa
upande wake, shahidi wa pili ambaye ni ofisa wa Takukuru, Redemta
Miremi alidai Februari 8, alimpokea mwananchi aliyemtaja kwa jina la
Marko Elias akidai kuelekezwa na mkuu wa wilaya kufika ofisi hizo kutoa
taarifa ya kuombwa rushwa.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )