TAMTHILIA ya Jumba la Dhahabu ndiyo iliyomtambulisha Miriam Jolwa ‘Jini
Kabula’ kwenye tasnia ya filamu kutokana na uigizaji wake mzuri.
Jina la Jini Kabula lilitokana na kuigiza kama joka kubwa,uwezo mkubwa
alioutumia katika kuigiza tamthilia hiyo iliwafanya watu wengi waamini
kwamba yeye ni jini kweli.
Katika hali ya kusikitisha, Jini Kabula alionekana hakuridhika na
umaarufu huo kwani baada ya tamthilia hiyo kupotea machoni mwa
Watanzania alianza kujiingiza kwenye ulevi, kuvaa nusu uchi na madai ya
kutoka kimahaba na baadhi ya wasanii wenzake wa kike.
Hata hivyo kwa sasa msanii huyo amekuwa kimya tofauti na miaka ya nyuma
ambapo alikuwa hakosekani kwenye magazeti mbalimbali nchini. Kitendo
hicho kilisababisha paparazi wetu kufunga safari ya kumtafuta kwa lengo
la kutaka kujua ukimya huo una heri?
Fuatilia…
Swagazz: Mbona upo kimya sana, hata kwenye magazeti hatuoni tena ukiandikwa kama zamani?
Jini Kabula: Kila jambo lina wakati wake, nimempata mwanaume ambaye
hataki mambo ya kijinga. Kwa kiasi fulani ni kama ufahamu wangu
umefunguka na sasa najuta kuwa maarufu, natamani kurejea hali yangu ya
kawaida lakini nashindwa.
Swagazz: Hee! Baadhi ya wasanii chipukizi wanasaka umaarufu kwa gharama
kubwa ikiwemo ya kutengeneza skendo ili waandikwe kwenye vyombo vya
habari na kurushwa kwenye mitandano ya kijamii, kulikoni?
Jini Kabula: Najuta kwa sababu kuna baadhi ya skendo huwa zinaandikwa
bila mimi kuzifanya hali ambayo huwa inasababisha nyumbani na jamii kwa
ujumla inichukie kutokana na matendo hayo.
Swagazz: Kuigiza kama jini kumeathiri vipi maisha yako?
Jini Kabula: Nimeathirika kwa sehemu kubwa sana. Wapo baadhi ya watu
mpaka sasa wanajua mimi ni jini kweli kutokana na urefu wangu, kuna
baadhi ya nyumba nyingine nikifika huwa wananikimbia huku watoto
wakipoteza fahamu kwa kuniogopa.
Kwa kweli hali hiyo inaniumiza sana japo wakati mwingine huwa nacheka tu
kwa kujua ujumbe nilioukusudia umeifikia jamii. Na hii ndiyo sababu
nasema nauchukia umaarufu kwa sababu wakati mwingine nakosa uhuru wa
kutembea kama watu wengine wasiojulikana zaidi kwenye jamii.
Mtanzania
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )