Mkurugenzi
Mkuu wa zamani wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (Rahco),
Benhadard Tito na wenzake wawili wamepadishwa kizimbani katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka manne.
Vigogo
wawili wa Rahco na mfanyabiashara wanakabiliwa na mashtaka ya uhujumu
uchumi, matumizi mabaya ya madaraka, kula njama na kusababisha hasara ya
dola za Marekani 527,540.
Mbali
na Tito, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwanasheria wa Rahco,
Emmanuel Massawe na mfanyabiashara ambaye pia ni mwakilishi wa kampuni
ya Rothschild (South Africa) Proprietary Limited, Kanji Mwinyijuma.
Washtakiwa
hao watatu walisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas
Simba, huku upande wa mashtaka ukiwa na Maghela Ndimbo, Janeth Machulya
wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kushirikiana
na Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis.
Mawakili
hao, wakiongozwa na Vitalis walidai kuwa washtakiwa wote watatu katika
nyakati tofauti kati ya Septemba Mosi, 2014 na Septemba 30, 2015 katika
Mkoa wa Dar es Salaam walikula njama ya kutenda makosa hayo chini ya
Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Katika
kesi hiyo, ilidaiwa kuwa Februari 27, 2015, Tito katika ofisi za Rahco
zilizoko wilayani Ilala, alitumia madaraka yake vibaya kwa kuipitisha
kampuni hiyo ya Rothschild kama mshauri wa mradi wa uimarishaji wa Reli
ya Kati bila idhini ya Bodi ya zabuni ya Rahco, hivyo kwenda kinyume na
Sheria ya Manunuzi ya Umma.
Tito
na Massawe wanadaiwa kuwa Machi 12, 2014 katika ofisi hizo za Rahco
walitumia madaraka yao vibaya kwa kutia saini barua rasmi ya kuichagua
kampuni hiyo, kama mshauri katika mchakato wa uimarishaji wa njia ya
Reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge).
Kati
ya Machi 12 na Mei 20, 2015 katika ofisi za Rahco, Tito na Massawe
wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kushindwa kuwasilisha mkataba
wa huduma ya ushauri, baina ya kampuni hizo mbili kwa Mwanasheria Mkuu
wa Serikali (AG).
Pia
wanadaiwa kuwa kati ya Mei 20 na Juni 20, 2015 katika ofisi hizo
washtakiwa hao, walishindwa kuwasilisha nakala ya mkataba kati ya
kampuni hizo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mbali
na mashtaka hayo, washtakiwa hao kwa pamoja kwa nyakati tofauti kati ya
Machi Mosi na Septemba 30, 2015 walitoa huduma ya ushauri kwa kampuni
hiyo, bila kufuata taratibu za ununuzi na malipo na walisababisha hasara
ya dola za Marekani 527,540 ambazo zililipwa kama gharama za malipo ya
awali.
Agosti
18, 2015, Tito akitekeleza majukumu yake, alitumia vibaya mamlaka kwa
kuipatia kampuni ya China Railway Construction Corporation kazi ya
ujenzi wa reli kwa kilomita mbili za kiwango cha kisasa kutoka Soga,
iliyogharimu dola Marekani 2, 312,229.39 bila ya kuwa na idhini ya bodi
ya zabuni ya Rahco.
Washtakiwa
hao hawakuruhusiwa kujibu kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya
kuisikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu. Uamuzi wa dhamana utatolewa
Ijumaa.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )