Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jijini Dar es Salaam, leo imefuta shtaka la utakatishaji fedha (money laundering) lililokuwa likimkabili Kamishna Mkuu Mstaafu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya sambamba na waliokuwa wafanyakazi wa Benki ya StanBic Tanzania, Sioi Sumari na Shose Sinare.
Awali watatu hao walikuwa wamenyimwa dhamana. Kutokana na uamuzi huo, mawakili wao sasa wanaweza kuwaombea dhamana.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), iliwafikisha mahakamani watatu hao April 1, kwa kisa la:- Kula njama na kujipatia kwa udanganyifu kinyume na kifungu Na. 384 cha Kanuni ya Adhabu (Cap 16 R.E. 2002) ; Kughushi kinyume na kifungu Na. 333,335 (a) na 337 cha Kanuni ya Adhabu (Cap 16 R.E 2002) ; Utakatishaji wa fedha haramu kinyume na kifungu Na. 12 (a) 13 (a) cha Sheria ya ya Utakatishaji fedha Na. 12 ya Mwaka 2006 ‘Anti- Money Laundering Act’.
Watuhumiwa hao walidaiwa kufanikiwa kujipatia fedha kwa njia ya kughushi dola milioni 6, kama malipo ya kufanikisha serikali ya Tanzania kupata mkopo wa dola milioni 550 kutoka Benki ya Stanbic ya Jijini London mkopo ambao ulipitia benki ya Stanbic tawi la Tanzania.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )