Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) inayohusu miradi inayosimamiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), imepelekwa kwa Rais Dk. John Magufuli kwa ajili ya kuipitia.
Awali ripoti hiyo ilitakiwa kuwasilishwa juzi kwenye Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge, baada ya wajumbe wa kamati hiyo kuiomba, lakini ilishindwa kuwasilishwa na viongozi wa NSSF kwa madai kuwa kuna tuhuma za ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za miradi mbalimbali inayosimamiwa mfuko huo.
Akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo juzi, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenister Mhagama, aliwaambia ripoti hiyo imetua mikononi mwa Rais Magufuli, hivyo hawawezi kuipata hadi aisome na kuiwasilisha bungeni.
“Kutokana na hali hii, kamati haiwezi kuipata ripoti hii hadi rais mwenyewe atakapoamua kuiwasilisha,” alisema.
Alisema kuna uwezekano mkubwa mjadala wa ripoti hiyo ukaendelea bungeni, baada ya Rais Magufuli kuipitia na kutoa maelekezo.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya kamati hiyo jana vilisema kuwa baada ya Waziri Jenister kutoa taarifa hiyo, wajumbe wa kamati walipinga na kuwataka watendaji wa NSSF waiwasilishe kwenye kamati hiyo kwa sababu wao ndio walioiomba ili waweze kuipitia na kuangalia utekelezaji wa majukumu ya mfuko huo.
Baada ya mvutano huo, Waziri Jenister alisisitiza taarifa alizonazo ripoti ipo kwa Rais, hivyo hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuipata hadi ipelekwe bungeni au atoe maelekezo mengine kwa kuwa yeye ndie mwenye kibali hicho kwa mujibu wa sheria.
Waziri Jenister alipotafutwa kuzungumzia suala hilo jana, alisema wizara yake haiwezi kulizungumzia kwa sababu liko mikononi mwa kamati.
Alisema kisheria ripoti ikifikishwa kwenye mikono ya rais, wizara haina mamlaka ya kujadili tena.
Wiki iliyopita, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohammed Mchengerwa, wakati akitoa majumuisho ya ziara walizofanya katika taasisi mbalimbali za Serikali na wizara, alisema walibaini kuwapo upungufu katika taarifa ya utekelezaji wa miradi mingi inayosimamiwa na NSSF.
Alisema kutokana na kasoro hizo, kamati iliona ni vema ikapata ripoti ya CAG ili ipitie na kujiridhisha kama miradi imetekelezwa au kuna harufu ya ufisadi.
“Kamati imebaini kuwepo nyumba nyingi zilizojengwa na NSSF ambazo hazikaliwi na watu, hali iliyotutia shaka. Inaonekana baadhi ya watu wamenufaika na miradi hii.
“Tunaamini miradi hii haijawanufaisha wanachama wake bali watu wachache, ndiyo maana tumeagiza ripoti ili tuipitie,” alisema Mchengerwa.
Alisema kutokana na hali hiyo, wameagiza kusimamishwa miradi mipya ya shirika hilo na kuiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Jamii (SSRA), kuhakikisha inasimamia ipasavyo mifuko pamoja na kuangalia miradi inayoanzishwa kama inawanufaisha wananchi na Serikali kwa ujumla.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )