Serikali
imesema itawafukuza kazi maofisa wa Serikali ambao wanaweka vikwazo na
kuwakwamisha waandishi wa habari kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa
kupata habari na taarifa mbalimbali kutoka serikalini.
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye aliyasema hayo
jijini Mwanza wakati alipozungumza na wadau wa utamaduni, habari na
michezo kutoka wilaya zote za mkoa wa Mwanza.
Alisema
hayo wakati akitoa ufafanuzi wa swali lililoulizwa na Mwandishi wa
Habari wa ITV/ Radio One anayefanyia kazi zake mikoa ya Kanda ya Ziwa,
Cosmas Makongo ambaye alitaka apate msimamo wa Serikali juu ya hatua
zitakazochukuliwa na serikali kutokana na wimbi la unyanyasaji wa
kijinsia unaofanywa na baadhi ya watendaji wa Serikali kwa waandishi wa
habari nchini.
Makongo
alisema akiwa wilayani Chato mkoani Geita hivi karibuni alizuiliwa
kuandika habari na ofisa mmoja wa Serikali hadi pale atakapopata kibali
kutoka kwa Mkuu wa Wilaya.
“Kumeibuka
wimbi la unyanyasaji wa kijinsia kwa waandishi wa habari, ukifika Chato
huandiki habari mpaka upate kibali kutoka kwa Mkuu wa Wilaya,
nilizuiliwa kuandika habari hivi karibuni wakati nafanya habari ya
uchunguzi wa mabilioni ya fedha wilayani humo,” alisema Makongo na kuhoji,
“Mheshimiwa Waziri tukiendelea kusubiri vibali kutoka kwa watawala je, tutafichua maovu?”
Nape
alisema kuwa msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John
Magufuli ni kuvitumia vyombo vya habari katika kufichua maovu
yanayofanywa na baadhi ya watu katika jamii.
“Kama
kuna Ofisa wa Serikali anaweka kizuizi kwa mwandishi wa habari ili
asipate habari na kushindwa kutimiza wajibu wake tutamfukuza kazi,” alisema Nape.
Aliwataka
maofisa wa habari kote nchini wawe tayari kutoa taarifa mbalimbali za
maendeleo zilizopo kwenye maeneo yao kwa wakati ili waandishi
wauhabarishe umma.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )