Wajumbe wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini (Alat), wanaotokana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamesusia uchaguzi kwa madai ya kuminywa kwa demokrasia.
Mkutano
huo uliofanyika jana katika ukumbi mpya wa CCM mjini Dodoma, wajumbe
wake ni wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri zote, mameya wa miji na
majiji na mbunge mmoja kutoka kila mkoa wa Tanzania Bara.
Nafasi zilizokuwa zikigombewa ni mwenyekiti, makamu wake na wajumbe 16 wa kamati ya utendaji.
Awali,
Mwanasheria wa Alat, Cleofas Manyangu aliwataja waliochukua na
kurejesha fomu za kugombea uenyekiti ni Gulam Mukadam (Meya wa
Shinyanga), Murshid Ngeze (Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bukoba
Vijijini), Chief Kalumuna (Meya wa Bukoba Mjini) na Isaya Charles (Meya
wa Jiji la Dar es Salaam).
Hata
hivyo, alisema waliokidhi vigezo kwa mujibu wa Katiba ya Alat, kanuni
za kudumu na mwongozo ni Mukadam na Ngeze wote kutoka CCM na waliosalia
wa Ukawa hawakukidhi.
Alisema
Charles na Kalumuna walishindwa kurejesha fomu katika muda uliowekwa wa
saa 6.00 mchana siku moja kabla ya uchaguzi na pia hawakupata wadhamini
10 kutoka kanda tano za Alat Taifa.
Kutokana
na kauli ya mwanasheria huyo, mwenyekiti wa muda wa mkutano huo ambaye
pia ni Meya wa Manispaa ya Dodoma, Jaffar Mwanyemba alitangaza kuwa
wagombea katika uchaguzi huo ni wawili.
Kauli
hiyo ilibadilisha hali katika ukumbi, huku wajumbe wa Ukawa wakitaka
wagombea wote waruhusiwe kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
Meya
wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro aliomba wagombea hao waruhusiwe kwa
kuwa maandalizi ya uchaguzi yalikiuka mwongozo, hali ambayo ilifanya
baadhi yao kutokidhi vigezo.
Alisema
taarifa ya mkutano huo ilitakiwa kuwafikia siku zisizopungua 28 kabla
ya uchaguzi, lakini wengi wao walipata barua hizo chini ya muda huo.
Akijibu
hoja hizo, Manyangu alisema taarifa za mkutano huo kwa mara ya kwanza
zilipelekwa kwenye halmashauri Novemba 2, mwaka jana.
“Tatizo
lililotokea ni baadhi ya halmashauri kuchelewa kukamilisha uchaguzi,
hali iliyosababisha mkutano kuahirishwa mara mbili,”alisema.
Baada ya hoja hizo, wajumbe wote wanaotokana na Ukawa walitoka nje ya ukumbi, huku wakiahidi kufanya kazi na Serikali Kuu pekee.
Akizungumza
nje ya ukumbi, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Charles alisema kutokana
na kuchelewa kwa uchaguzi jijini humo hakupata taarifa mapema kuhusu
mkutano na uchaguzi huo.
Hata hivyo, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe na meya wa Manispaa ya Kigoma walishiriki uchaguzi kama kawaida.
“Mimi sijui chochote. Sijui wametoka kwa sababu gani maana nimefika hapa nikiwa nimechelewa,” alisema Zitto.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )