Rais
Uhuru Kenyatta wa Kenya aliondoka nchini mwake jana asubuhi kwenda
Ufaransa na Ujerumani kwa ziara ya kazi ambayo pamoja na mambo mengine
itahusisha suala la ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda.
Kenya
hivi karibuni imeingia katika mvutano na Uganda, ikiitaka jirani yake
huyo kurudisha mpango wa kulipitisha bomba hilo la mafuta nchini humo
(Kenya) badala ya Tanzania.
Suala hilo ni sehemu ya ajenda ya biashara, ushirikiano na maendeleo ambayo ni moja ya malengo ya ziara ya Rais Kenyatta.
Kituo
cha kwanza cha ziara ya Rais Kenyatta kitakuwa Paris, Ufaransa,
kuanzia leo Aprili 4 hadi 6 kabla ya kuelekea Berlin, Ujerumani
atakakokaa hadi Aprili 8, mwaka huu.
Itakuwa ni mara ya kwanza katika miaka 17 kwa Rais wa Kenya kuitembelea Ujerumani.
Mara
ya mwisho, ziara ya aina hiyo ilifanywa na Rais Daniel arap Moi mwaka
1999 huku Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, akiitembelea Kenya mwaka
2011.
Ziara nchini Ufaransa kwa mujibu wa Ikulu ya Kenya, imeandaliwa na wizara ya mambo ya nje kwa mwaliko wa Rais François Hollande.
Ziara
ya Ufaransa inatarajia kuipa Kenya fursa ya kuzungumzia suala la ujenzi
wa bomba la mafuta kutoka Uganda, ikilenga kuiomba serikali ya nchi
hiyo kutia mkono wake kufanikisha azma yake ya ujenzi wa bomba hilo.
Kenye inahesabu imeporwa na Tanzania mradi huo.
Kampuni
ya Total ya Ufaransa ni mwanahisa mkubwa wa uwekezaji wa mafuta Uganda
na inaaminika ndiyo iko nyuma ya uamuzi wa hivi karibuni wa Uganda
kuachana na mpango wa ujenzi wa bomba hilo kutoka njia ya Hoima-
Lokichar- Lamu ya Kenya na badala yake kulijenga hadi katika bandari
ya Tanga, Tanzania.
Tofauti
na washirika wengine wa uwekezaji huo kutoka Uingereza na China, Total
mara kwa mara imekuwa ikisisitiza ujenzi wa bomba hilo kupitia njia ya
Kusini nchini Tanzania kwa kile inachosema unafuu na usalama
kulinganisha na Kenya.
Tayari
mmoja wa viongozi wake waandamizi amemtembelea Rais John Magufuli
Ikulu, Dar es Salaam na kumhakikishia dhamira ya kampuni hiyo pamoja na
kupatikana kwa fedha za ujenzi huo.
Kampuni
hiyo pia imetoa tamko jingine hivi karibuni wakati wa mkutano wa wadau
wa nishati Afrika Mashariki uliofanyika Dar es Salaam, ikisema inajua
jitihada zinazofanywa na Kenya kutaka bomba hilo lijengwe nchini humo,
lakini msimamo wake wa kujengwa Tanzania uko pale pale.
Kwa mujibu wa taarifa za Ikulu, Ufaransa iko katika nafasi ya sita kama mmoja wa wawekezaji wakubwa Kenya.
Uwekezaji
huo unaanzia sekta ya uchukuzi, ufamasia, magari na sekta ya huduma
zikiwamo SDV-Transami, AGS, Frasers Schneider, Peugeot, Renault,
Michelin na Proparco.
Wawekezaji
wengine ni Total Kenya, Bamburi Cement, Alcatel, na kampuni ya
mawasiliano ya Ufaransa Telecom yenye ubia na Telkom Kenya na Orange
Mobile.
Kwa mujibu wa mpango wa ziara nzima, Rais Kenyatta akiwa Ujerumani atakuwa na mkutano na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )