Wabunge wa CCM jana waliibuka kidedea walipowazidi wenzao wa upinzani kwa kura za sauti “Siyooooo” kuikataa hoja ya kutaka matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja ‘live’ na televisheni.
Hiyo
ilitokea jana wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha bajeti ya
Ofisi ya Rais (Tamisemi na Utumishi na Utawala Bora) na kuzua mvutano
mkali uliosababisha bajeti hiyo ipitishwe kwa utaratibu wa wabunge
kutohoji kitu chochote (guillotine).
Wakati
hoja yao hiyo ikipingwa kila kona, tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti,
wabunge hao wa upinzani sasa wamebuni mbinu mpya ya kujirekodi wenyewe
wakati wakichangia mijadala mbalimbali bungeni na kurusha sauti zao
kwenye mitandao ya kijamii na kupeleka sauti hizo kwenye redio zilizopo
katika maeneo ya majimbo yao.
Mbunge
wa Malindi (CUF), Ally Salehe ndiye aliyeibua hoja hiyo akitaka kushika
mshahara wa waziri kwa maelezo kuwa kuzuia Bunge kurushwa ‘live’ ni
kinyume na utawala bora na haki ya kupata habari.
Hoja
hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji
Peter Msigwa, Masoud Abdalla Salim (Mtambale-CUF), Rose Kamili (Viti
Maalumu -Chadema), Ester Matiko (Tarime Mjini – Chadema) na Mussa
Mbarouk (Tanga Mjini - CUF).
Wabunge
wa CCM waliopewa nafasi na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kuchangia
hoja hiyo ni Peter Serukamba (Kigoma Kaskazini), Kangi Lugola
(Mwibara), Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini) pamoja na Waziri Ofisi ya Rais -
Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki.
Ilivyokuwa Bungeni
Baada
ya Salehe kutaka ufafanuzi wa kina huku akisisitiza kuwa uamuzi huo
unakiuka Katiba ya nchi na haki ya kupata habari, Kairuki alisema kwa
mujibu wa Ibara ya 18 na 100 ya Katiba zinazozungumzia uhuru wa kupata
habari, uamuzi huo ni sahihi na hakuna mwananchi aliyenyimwa taarifa.
Maelezo
hayo yalipingwa na Salehe, safari hii akifafanua kuwa matangazo ya
Bunge yanarekodiwa kwa saa saba na kurushwa na Televisheni ya Taifa
(TBC) kwa saa moja tu, huku wabunge wa upinzani wakiondolewa na
kuonyeshwa wa CCM pekee.
Alitaka
vyombo vya habari vya elektroniki kuruhusiwa kurekodi shughuli za Bunge
na kurusha maudhui wanayoyataka, badala ya kupewa video na studio ya
Bunge ambayo huondoa michango na hoja za wapinzani.
Mchungaji
Msigwa, Masoud Abdallah, Kamili, Matiko waliungana na Salehe na
kusisitiza kuwa nchi nyingi barani Afrika zinarusha ‘live’ matangazo ya
Bunge huku wakihoji sababu za TBC kurusha moja kwa moja harusi na
kushindwa kuonyesha shughuli za Bunge.
Mbarouk
alikwenda mbali akitaka Bunge kuanza shughuli zake usiku ili kuendana
na utetezi wa Waziri wa Habari, Nape Nnauye kuwa usiku wananchi wengi
wanakuwa majumbani mwao hivyo wanapata nafasi nzuri ya kufuatilia Bunge.
Matiko: Juzi
Rais John Magufuli kazindua Daraja la Kigamboni, TBC ilikata matangazo
ya Bunge ili kuonyesha uzinduzi huo. Yaani ya kwenu mnataka yaonyeshwe
ila haya ya Bunge yasionekane. Mnakiuka demokrasia.
Ghasia: Demokrasia siyo Bunge kuonyeshwa ‘live’. Wakulima na wafugaji hawawezi kuona Bunge asubuhi ndiyo maana yanarushwa usiku.
Serukamba: Mbona
wabunge wa Chadema wanaonyeshwa katika matangazo ya TBC. Hoja kwamba
maagizo ya Serikali hayatawafikia watendaji si kweli.
Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju alisema wapinzani hawajiamini na
hawaaminiki huku akiwataka wasome ibara ya 100 ya Katiba; “Bunge kuonyeshwa au kutoonyeshwa hakuongezi kitu jimboni. Wanaozungumza ni wabunge siyo televisheni.”
Akihitimisha hoja, Kairuki alipinga maelezo ya Salehe na kutoa mfano wa nchi ambazo matangazo ya Bunge hayarushwi moja kwa moja.
Kutokana
na mvutano huo Chenge aliwahoji wabunge wanaoafiki hoja ya Salehe
waseme “ndiyooo”, wapinzani pekee wakasema ndiyoo, aliposema wasioafiki
waseme siyo, wabunge wa CCM kutokana na wingi waliitikia kwa sauti kubwa
siyoooo, na Chenge akasema anadhani wasioafiki wameshinda.
Wapinzani Waamua Kujirekodi kwa simu
Kwa
zaidi ya mara tano,wabunge wa upinzani wameshuhudiwa wakijirekodi ndani
ya ukumbi wa Bunge kwa kutumia simu zao za mkononi, wanapotoka nje
huulizana kama wameshatumia video na sauti hizo katika mitandao ya
kijamii.
Juzi,
Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara baada ya kumaliza kuchangia
mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais (Tamisemi na Utawala Bora) alirusha
sauti yake katika mitandao ya kijamii na kusema hiyo ni moja ya njia ya
kuwafanya wananchi wajue kinachoendelea bungeni.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )