Featured
Loading...

Noti na Sarafu za Shillingi 500 zatoweka



NOTI na sarafu ya Sh 500 zimeadimika kwenye mzunguko wa fedha kwa zaidi ya mwezi sasa, hali inayosababisha adha kubwa kwa wafanyabiashara,imefahamika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti   mwishoni mwa wiki, baadhi ya wafanyabiashara na makondakta wa mabasi ya daladala, Dar es Salaam, walieleza kuwa kukosekana kwa noti na sarafu ya Sh 500 kunasababisha usumbufu na kuongeza ugumu   katika kurudisha chenji kwa wateja.

Majidi Seifu ambaye ni kondakta wa daladala linalofanya kazi kati ya Kariakoo na Temeke, alisema mbali na kuadimika, noti za 500 zilizopo kwenye mzunguko zimechakaa kwa kiasi kikubwa.

“Noti na sarafu ya Sh 500 imekuwa ngumu kupatikana na kusababisha usumbufu mkubwa kwetu na abiria hususan wakati wa asubuhi.

“Hutulazimu kununua chenji kwa gharama kubwa na kutusababishia hasara  na uchelewaji vituoni,” alisema Seifu na kuongeza:

“Kama ukibahatika kupata noti hiyo inakuwa imechakaa sana na hata ukimpa abiria anaikataa huku  wauza chenji wakipandisha kiwango kutoka  Sh 4,500 hadi  Sh 4,700 kwa noti ya Sh 5000,” alisema Seif.

Mfanyabiashara wa kuuza chenji katika eneo la  Kariakoo, Orimpora Hussein, alisema  upatikanaji wa fedha hizo kwa kwa sasa ni mgumu tofauti na awali kwa vile  inaweza kupita siku siku nzima bila kushika noti wala sarafu ya Sh 500.

“Kawaida kuuza chenji ndogo kama 100 au 200 kwa  Sh 1,000 unauza kwa Sh 800 na chenji ya  50 au 100 ni Sh 700  ikiwa ni bei ya kawaida.

“Kutokana kuadimika kwa noti na sarafu hizo ni fursa kwetu maana chenji ya Sh 5,000 tunauza kwa Sh 4,500 na fedha hizo naona zinazidi kupotea katika mzunguko wa kila siku,” alisema Orimpora.

Alipoulizwa kuhusu hali hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Benki kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Marcian Kibello, alisema noti za Sh 500 hazitakuwapo katika mzunguko wa fedha kwa vile hazitatengenezwa tena.

“Tangu tulipoitambulisha sarafu ya Sh 500 Oktoba 2014 hatujatengeneza noti tena kwa sababu  zinachakaa na kuharibika mapema ingawa wananchi wanazikataa sarafu.

“Ila sarafu zinapunguza gharama kwa vile zinadumu tofauti na   noti.

“Nashauri taasisi za fedha kuhakikisha zinasambaza sarafu hizo katika mzunguko wa fedha na pia wananchi wazizoee kwa matumizi na  wazichukue sarafu hizo katika benki mbalimbali  kuhakikisha zinakuwapo katika mzunguko,”alisema Mkurugenzi huyo.

Kibello aliwakumbusha wananchi kuwa BoT inatoa huduma ya chenji za sarafu ya Sh 500 kila siku za Jumanne na Alhamisi hivyo wananchi na wafanyabiashara watumie fursa hiyo kuzipata.

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top