Msichana wa kidato cha Nne mwenye umri wa miaka 17,(jina tunalo) anayesoma shule moja ya sekondari ya Kata mkoani Mbeya amekumbwa na kadhia ya kuvuliwa nguo zake za ndani na kucharazwa bakora zisizo na idadi na walimu wanne wa shule hiyo.
Tukio hilo ambalo limeripotiwa katika kituo kidogo cha Polisi Mbalizi wilaya ya Mbeya kwenye jalada la uchunguzi namba MBI/IR/967/2016 na kuwekwa kwenye taarifa yenye namba MBI/RB/2653/2016 linadaiwa kuwahusisha walimu wanne akiwemo Mkuu wa shule hiyo pamoja na walimu watatu.
Akizungumza huku akiwa na maumivu makali katika Hospitali Teule ya Ifisi ambako amelazwa akipatiwa matibabu, mwanafunzi huyo alisema kuwa aliitwa na mwalimu wa nidhamu aliyemtaja kwa jina la Neema Mwaikenda aliyekuwa pamoja na Mkuu wa shule hiyo aliyemtaja kwa jina la Mariamu Mwanisenga na mwalimu wa kiume aliyemtaja kwa jina la Adili.
Alisema walimu hao walianza kumuadhibu kwa viboko visivyo na idadi huku akiwa amechojolewa nguo zake ambapo mwalimu wa kiume aliyemtaja kwa jina la Adili akaanza kumshikashika sehemu zake za siri.
‘’Wakati naadhibiwa na walimu wote, huyu mwalimu wa kiume alianza kunishika huku chini,na kunitaka niwataje wanaume zangu,nikawa nabana miguu wakazidi kunishambulia kwa vibao na mateke na fimbo,’’alisema mwanafunzi huyo.
Alisema sababu zilizosababisha aadhibiwe ilikuwa ni utoro na kuwa siku moja alipokuwa shuleni alioneshwa na walimu fimbo na kuelezwa kuwa fimbo hizo zitamuishia mwilini ndipo akaogopa kufika shuleni kwa siku tatu.
Anafafanua kuwa siku aliyofika shuleni ndipo alipokutana na kadhia ya kupigwa na walimu wanne hadi alipowaponyoka walimu hao na kukimbilia mitaani na kujificha.
‘’Niliwaponyoka walimu nikakimbilia kwenye nyumba ya jirani na shule nikajificha hadi jioni na baadaye kwenda nyumbani, kesho yake mama na dada walinichukua na kunileta hospitali,’’alisema.
Mwandishi wa habari hizi alifika shuleni anakosoma mwanafunzi huyo kwa nia ya kukutana na uongozi wa shuleni hiyo ambapo Makamu Mkuu wa shule hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Mwansanga alikataa kuelezea chochote.
‘’Mie sijui lolote kwanza mie sio msemaji wa shule, kwahiyo sijui lolote juu ya taarifa mnazohitaji,’’alijibu Makamu Mkuu wa shule na kuondoka zake.
Kwa upande wake Ofisa Elimu wa Mkoa Charles Mwakalila alisema kuwa adhabu aliyopewa mwanafunzi huyo ni kubwa kupitiliza kwa kuwa zipo taratibu za adhabu kulingana na makosa na kuwa mwanafunzi anapaswa kupigwa viboko vitatu na viboko visivyozidi sita au adhabu mbadala.
‘’Adhabu aliyopewa ni kubwa, tutafuatilia na waliokiuka taratibu watachukuliwa hatua za kinidhamu,’’alisema Mwakalila.
Naye Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mbeya Dhahiri Kidavashari alipoulizwa juu ya tukio hili alidai kuwa halijafika ofisini kwake na kuwa kwa sasa yeye yupo kikazi wilayani Chunya na mara atakapofika ofisini atafuatilia na kuchukua hatua za kisheria kwa wahusika wa tukio hilo.
Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya Mariamu Mtunguja ambaye alifika Hospitalini alikolazwa mwanafunzi huyo alisema kuwa amemuangalia mwanafunzi huyo na kuona namna ambavyo damu imevilia kwenye sehemu zake za makalio na kwenye mapaja.
Mtunguja alisema kuwa kitendo kilichofanywa na walimu hao ni cha kinyama ambacho hakipaswi kuvumiliwa na kuwa mara itakapobainika atahakikisha walimu hao wanachukuliwa hatua za kinidhamu.
Muuguzi Mkuu Msaidizi wa Hospitali Teule ya Ifisi Elimati Sanga alisema kuwa mwanafunzi huyo alifikishwa hospitalini hapo Julai 21 saa 7:00 mchana ambapo alipatiwa matibabu na kulazwa kutokana na majeraha na damu iliyovilia mwilini sehemu za makalio na mapaja.
‘’Ameshambuliwa sehemu za mapaja, damu na masikio yake hasikii vyema kutokana na kipigo, anaendelea na matitabu hapa hospitali,’’alisema Sanga.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )