Katika taarifa yake fupi kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana, Lowassa amewahakikishia wananchi kuwa kwa sasa ana “ari, nguvu na hamasa kuliko wakati mwingine wowote”.
Lowassa, ambaye alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, alijiondoa kwenye chama tawala Julai 28 mwaka jana baada ya jina lake kuondolewa kwenye orodha ya wagombea urais kwa tiketi ya CCM.
Kuondoka kwake kulisababisha mawaziri wa zamani, wabunge, wenyeviti wa mikoa, madiwani na wanachama wengine wa CCM, wakiongozwa na waziri mwingine mkuu wa zamani, Frederick Sumaye kukihama chama hicho, hali iliyosababisha ushindani kuwa mkubwa kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, huku CCM ikilalamikia kusalitiwa.
Wakati CCM ikifikiria hatua za kuchukua dhidi ya wasaliti wa chama wanaotuhumiwa kuunga mkono harakati za upinzani wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, Lowassa ameongeza petroli kwenye moto ulioanza kuwaka.
“Kwa wale wenzangu waliobaki CCM na wanaoniunga mkono, tuendelee kushikamana na kunipatia taarifa kwa hatima ya nchi yetu,” amesema Lowassa ambaye kwa sasa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.
“Nawashukuru Watanzania kwa kuendelea kuniunga mkono mimi na wenzangu ndani Chadema.”
Kauli hiyo kuwa kuna watu ndani ya CCM ambao wanampatia taarifa mbunge huyo wa zamani wa Monduli na ombi lake la kutaka waendelee kumpa taarifa, inaweza kusababisha hali ngumu zaidi kwa chama hicho, ambacho kinaamini kuwa makada wake walikihujumu wakati wa uchaguzi kwa kumfanyia kampeni kisiri.
Katika uchaguzi huo, Rais John Magufuli alishinda kwa kupata asilimia ndogo ya kura kulinganisha na watangulizi wake.
Ingawa alipata kura milioni 8.8 na Lowassa kufuatia kwa kupata kura milioni 6.07, ushindi huo ni wa asilimia 58.46 dhidi ya asilimia 39.67 kulinganisha na ushindi wa asilimia 61.17 aliopata Kikwete mwaka 2010 dhidi ya asilimia 26.34 alizopata Dk Willibrod Slaa wa Chadema.
Tangu Januari mwaka huu, CCM imekuwa ikijadili wasaliti hao katika ngazi ya wilaya na taarifa za mapendekezo ya hatua dhidi yao kutumwa Halmashauri Kuu kwa ajili ya uamuzi wa mwisho.
Katika hotuba yake ya kuaga, Jakaya Kikwete alimkabidhi mwenyekiti mpya wa CCM, Rais Magufuli ripoti ya hali ilivyokuwa kwenye uchaguzi, akisema yeye ndiye atakayeamua adhabu dhidi ya wale wote walioonekana kufanya makosa. CCM imeshasema kuwa wasaliti wote ni lazima washughulikiwe.
Katika taarifa yake ya jana, Lowassa ameeleza kuwa uamuzi alioufanya wa kuihama CCM na kujiunga na Chadema “haukuwa rahisi, lakini kwa ushupavu, ujasiri na mwongozo wa Mungu nilifanya hivyo” na kwamba huo ni “uamuzi wa kihistoria katika nchi yetu.
“Najivunia kwa uamuzi ule, kwani umewafungua macho Watanzania wengi na kuimarisha demokrasia. Nimeingia Chadema nimewakuta viongozi na wanachama walio na moyo wa dhati wa kuliletea maendeleo Taifa lao kivitendo,” anasema Lowassa katika taarifa yake fupi.
“Watanzania bado wanataka mabadiliko na imezidi kuthibitisha kuwa hawawezi kuyapata ndani ya CCM. Watanzania wanataka sera na mtu mbadala wa kuongoza mabadiliko hayo. Vyote hivyo watavipata ndani ya Chadema na Ukawa kwa jumla.”
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )