Featured
Loading...

Faida Za Uwekezaji Wa Majengo Kwenye Maeneo Salama Na Yaliyopimwa Na Wataalam Wa Ardhi


Asante mungu uliye mkuu na mwenye mamlaka juu ya viumbe vyote vya ulimwengu huu nami nitakutukuza na kukuabudu kwa uumbaji wako na pale tunaposhindwa wanadamu wewe ndipo unapoanzia.

Baada ya kumshukuru muumba wetu narudi kwako msomaji wangu, Hali ya uwekezaji wa majengo inazidi kukua kwa kasi hapa Tanzania na kuna mwamko mkubwa wa watanzania na wengi wao wameamua kwa moyo mmoja kufanya maamuzi mazito na ya kijasiri kwenda sambamba na uwekezaji wa ardhi na majengo.

Tatizo kubwa ambalo nimekutana nalo ni kwamba watanzania wengi bado hawajapata elimu ya upimaji wa maeneo ya uwekezaji na hawafahamu wafanye nini, hali hii ni hatari kwa kila mwananchi na taifa ikiwa kila mtu atajenga vile apendavyo na mahali popote pasipo kuzingatia sera na sheria za ujenzi za nchi. Hii ndiyo sababu kubwa ya majiji yetu kuwa machafu kupindukia na mahali pasipo na usalama wa kuishi kwa raia na mali zao.

Zaidi ya 80% ya majengo ndani ya majiji yetu yamejengwa kiholela na yanatambulika kama makazi holela. Kiini cha tatizo hili ni kushindwa kwa wizara ya ardhi kupitia halmashauri zake kupanga miji (rural and urban master-plan) na kuwapimia wananchi maeneo yao ili kuendana na kasi kubwa ya maendeleo na ongezeko kubwa la watu mijini na sehemu mbalimbali za kuzalisha uchumi.

Hata hivyo Lengo la makala hii ni kukuwezesha kutambua faida ya uwekezaji wa majengo kwenye maeneo salama na yaliyopimwa na wataalam wa ardhi, haya ni mambo ambayo watu wengi hawayajui kutokana na kukosa taarifa sahihi.

1. Haki halali ya umiliki wa ardhi kisheria 
Ujenzi wa majengo kwenye maeneo yasiyopimwa na ambayo hayakuratibiwa na halmashauri za mipango miji huwa katika wakati mgumu endapo litatokea tatizo lolote linalohusiana na ujenzi huo au baada ya jengo hilo kukamilika. Huwa na wakati mgumu hata wa kufanya utetezi wa aina yeyote kwa kuwa hakuna sera au sheria ya kusimamia jambo hilo.

Ingawa kwa Tanzania majengo yaliyojengwa kiholela yametambuliwa na baadhi kupewa leseni za makazi. Hata hivyo ni vema ukajenga kwenye maeneo yaliyopimwa ili uwe salama wakati wote kwa kuwa ujenzi hugharimu fedha nyingi, hivyo huna sababu ya kujenga nyumba ya kudumu maeneo yasiyo salama.

Kwenye maeneo yaliyopimwa kila mmiliki anapewa hati halali ya umiliki wa kipande cha ardhi ndani ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sera na sheria za ardhi. Ni rahisi sana kueleweka na kupata msaada wowote na mahali popote ukiwa na hati miliki ya ardhi. Umiliki huo huhifadhiwa kwenye mfumo wa kisasa (data-base) ambayo hutambua umiliki wa kila kipande cha ardhi kilichopimwa na kusajiliwa. Pia ni rahisi kulipwa fidia halali na halisi kwa thamani ya wakati huo endapo ardhi hiyo itahitajika na jamhuri kwa matumizi mengine na kulazimika kuondoka mahali hapo.

2. Uhakika wa sehemu sahihi ya uwekezaji 
Ujenzi wa majengo kwenye maeneo maarufu kama “skwata” una faida na taabu zake. Lakini faida huwa ni chache kuliko taabu azipatazo mkazi wa maeneo hayo. Maeneo haya hujengwa pasipo kufuata taratibu za aina yeyote ile zinazohusiana na ujenzi au manunuzi ya maeneo hayo. Hakuna mpangilio maalumu wa uuzaji wa maeneo matokeo yake kila mtu anajenga kulingana na ufahamu wake na anajenga atakavyo. Sehemu sahihi ya uwekezaji ni eneo maalumu kwa ajili ya uwekezaji wa aina fulani na si vinginevyo.

Maeneo ya makazi yajengwe makazi ndivyo hivyo na viwanda vijengwe kwenye maeneo ya viwanda na si vinginevyo. Huu ndio umuhimu wa kuwa na “master plan” ya miji na majiji. Ni rahisi kwa kila mwananchi kufahamu aende wapi na anunue na kujenga wapi katika kutimiza dhamira yake ya kibinadamu.

Hakuna furaha ya kweli ikiwa umejenga nyumba yako ya kuishi na jirani yako amejenga baa inayokesha usiku wote kwa kelele za muziki ili hali wewe unahitaji kupumzika ili kesho uendelee kutimiza majukumu yako ya kila siku au jirani ya nyumba yako kimejengwa kiwanda kinachotoa moshi siku zote za uzalishaji wake. Unaponunua maeneo yasiyopimwa hujui jirani yako atajenga nini na atajenga kwa mwelekeo upi ili akujali wewe, tafadhali tafakari na fanya maamuzi sahihi.

3. Uhakika wa miundombinu bora na salama 
Nyumba nyingi zilizojengwa kwenye makazi holela zipo kwenye kila aina ya taabu na kero za kibinadamu. Hata nyumba iwe kubwa na nzuri kiasi gani bado inakuwa ipo kwenye hatari kubwa ya kuhimili mazingira salama ya jengo hilo na kukidhi haja maalumu ya kibinadamu.

Na wakazi wa nyumba hizo pia huwa katika mazingira hatarishi kutokana na kutokufikiwa na miundombinu bora na salama inayokidhi mahitaji muhimu ya kibinadamu. Mfano, Nyumba iliyo umbali wa mita Zaidi ya 500 kutoka kwenye barabara baada ya hapo ni chochoro kila upande hadi kuifikia nyumba hiyo mara nyingi maeneo hayo huchochea mazingira ya uhalifu wa kila aina, uchafuzi wa mazingira na kutofikiwa kwa baadhi ya miundombinu ya lazima.

Maeneo haya umeme hupita juu ya mapaa yao ya nyumba kuelekea sehemu tofauti, mabomba ya maji safi yanapita pembezoni mwa vyoo au kuchanganyana na mfumo wa maji taka. Taka ngumu huzagaa kila mahali kwa kuwa hakuna eneo maalumu linalotengwa kwa ajili hiyo. Pia huwa hatari zaidi endapo litatokea janga la moto na usalama wa raia na mali zao huwa ni mdogo sana. Epuka taabu na dhahma hizi kwa kujenga sehemu salama na uweze kufurahia maisha ya uwekezaji wako kwa kuwa kila nyumba inafikika kwa uhakika.

4. Huchochea mazingira bora ya uwekezaji 
Kukosekana kwa miundombinu ya barabara, mawasiliano nishati umeme, mfumo wa maji safi na maji taka kwenye eneo fulani husababisha kudumaa kimaendeleo na kifikra kwa wakazi wa maeneo hayo. Hii ni kutokana na wakazi wa maeneo hayo kuzingirwa na mazingira yasiyo rafiki kwa maendeleo ya kibinadamu. Hakuna eneo safi la kupumzika, kelele za muziki kila kona, hakuna eneo la kucheza na kukua kwa watoto na mengine mengi.

Maeneo haya maarufu kwa jina la “uswahilini” kuna kila aina ya vitimbi kutokana na kukosekana kwa miundombinu rafiki kwa ajili ya kuchochea maendeleo. Maeneo yaliyopimwa ni rafiki wa binadamu na maendeleo yake ya kiuchumi na kijamii, pia huchochea kila aina ya maendeleo endapo wakazi wa maeneo hayo watapata hamasa ya kufanya maendeleo makubwa kwa kuwa wana fursa zote za kimafanikio zinazo chochewa na miundombinu chanya iliyopo.

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top