Ndugu zangu,
Kabla ya
kwenda Zanzibar kwa mara ya kwanza mwaka 1989, nilisoma habari nyingi za
kihistoria juu ya watu wa visiwa hivyo. Nilisoma pia historia ya
mapinduzi yao ya mwaka 1964.
Nakumbuka
nilisafiri na jahazi lililojengwa kwa mbao liitwalo Ras Nungwi. Safari
ilichukua saa nane majini, maana jahazi lilijaza shehena kubwa ya
magunia ya chumvi.
Enzi hizo
Zanzibar jahazi halikufika mpaka kwenye gari kutia nanga. Tulisubiri
mbali na gatini na ikaja mitumbwi midogo kutuchukua abiria. Ilikuwa ni
kuurukia mtumbwi kutoka jahazini. Ukiuokosa na kuangukia majini, basi,
ni lazima uogelee!
Basi,
nikiwa kisiwani Unguja nikatamani nifike kisiwa kidogo cha Tumbatu.
Kutoka Mikokotoni Unguja hakuna umbali mrefu kufika Tumbatu kwa mtumbwi.
Ni kisiwa
kidogo chenye urefu wa takribani kilomita nane, na mapana ya kilomita
mbili. Niliwaona Watumbatu wakiwa tofauti sana na Waunguja.
Watumbatu,
kwa mtazamo wangu hata wa wakati huo nikiwa kijana mdogo sana,
niliwaona kuwa ni watu wenye usiri mkubwa. Kwanza walionekana kushangaa
iweje kijana mdogo kutoka bara na wala si Unguja nimekwenda kutaka kujua
habari zao.
Na ugumu ukawa pia kwangu kufahamu wanachoongea, waliongea labda niseme Kibantu cha Kitumbatu. Niliwaelewa, lakini kwa tabu.
Hata
wakati huo, Watumbatu walionyesha kuwa wao ni tofauti na Waunguja,
kwamba Tumbatu ni ya Watumbatu. Hawakutaka kuyazungumzia sana ya Unguja,
na waliona kuwa ni mbali na kwao, hata kama ni umbali wa kilomita
kadhaa tu.
Kwa
mashaka, Watumbatu walinikaribisha makwao na hata chakula na maji ya
kunywa. Muda mwingi nilihisi wakinihofia , kuwa ni mtu niliyetumwa jambo
kwao.
Mwishowe, wanawake wa Kitumbatu ni warembo sana, as'kwambie mtu..!
Maggid, (P.T)
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )