Mwenyekiti
wa TLP, Augustino Mrema amesema pamoja na Rais John Magufuli kufanya
kazi vizuri, hawezi kurejea CCM na badala yake amependekeza vyama hivyo
viwili viunde ushirikiano wao kama ilivyo kwa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa).
Waziri
huyo wa zamani wa mambo ya ndani, pia amesema kuna haja ya suala la
maandamano na mikutano ya kisiasa kuundiwa kanuni ili kuondoa malalamiko
ya vyama vya upinzani kuzuiwa kutekeleza haki hiyo ya kikatiba.
Mrema,
ambaye hivi karibuni aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa mwenyekiti wa
Bodi ya Msamaha kwa Wafungwa (Parole), alitoa kauli hiyo jana wakati
akihojiwa kwenye kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na kituo cha
redio cha Clouds FM.
Alikuwa
ameulizwa na mmoja wa wasikilizaji wa kipindi hicho kwa nini asirejee
CCM kama anaridhika kuwa Rais Magufuli anatekeleza yale ambayo alitaka
yafanyike lakini hayakufanyika hadi akaamua kuisaliti Serikali ya Awamu
ya Pili na kuihama CCM na kwenda NCCR-Mageuzi kabla ya kuanzisha chama
cha TLP.
Mrema
alijibu swali hilo kwa kuanza kueleza historia yake na mambo aliyofanya
wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani katika kupambana na uhalifu na
kwamba alipoona anatofautiana na Serikali aliamua kujitoa.
Alisema
CCM chini ya Serikali inayoongozwa na Rais Magufuli inafanya vizuri kwa
kutekeleza yale aliyokuwa akiyataka wakati akiwa waziri.
Alisema
Rais Magufuli anatoa ushirikiano kwa kila mtu, hivyo atakuwa bega kwa
bega kumsaidia kiongozi huyo aliyedai anatekeleza majukumu yake kwa
uwazi.
“Hiyo Ukawa nyingine siipendi kwa sababu haijui inataka kufanya nini.”
Mrema,
ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Vunjo kwa tiketi ya TLP mwaka 2010
hadi 2015, alisema ataendelea kumwamini Rais Magufuli kutokana utendaji
kazi wake kazi mzuri, ikiwamo kupambana na ufisadi, kazi ambayo alisema
anapenda aone ikifanyika.
Akizungumzia
uamuzi wa Rais Magufuli kupiga marufuku maandamano na mikutano ya
kisiasa, Mrema alisema agizo hilo ni sahihi kwa sababu hakuna haja ya
mikutano wakati uchaguzi ulishapita.
Lakini
alipoulizwa kama Serikali ingezuia mikutano na maandamano wakati
alipoihama CCM mwaka 1995, Mrema, ambaye alivuta hisia za wengi wakati
huo alisema katika kipindi hicho Rais hakuwa Magufuli.
Alisema
kama Magufuli angekuwa ni Rais wakati huo na anatekeleza hayo aliyokuwa
anataka, angekubaliana na uamuzi wa kuzuia maandamano.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )