Mwenge wa uhuru utawasili leo Nyamagana ukitokea Sengerema mkoani Mwanza na tayari umeibua hisia kali baada ya wananchi kutakiwa kutoendelea na shughuli zao za kujiingizia kipato na kuhudhuria mapokezi yake.
Gari la Jiji la Mwanza limepita asubuhi ya leo na kuwatangazia wananchi wote kusitisha shughuli zao kwa madai kuwa leo ni sikukuu ya Nanenane na mwenge wa uhuru huku barabara ya Nyerere inayounganisha Jiji la Mwanza ikifungwa kabisa.
Amri ya kusitisha shughuli zote ili kuhudhuria mapokezi ya mwenge wa uhuru inadaiwa kutolewa na DC Tesha huku gari mali ya jiji la Mwanza ikizunguka kutoa matangazo hayo.
Julai 3, mwaka huu, DC Tesha pia anadaiwa kuwaita ofisini kwake walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari wilayani humo na kuwataka kuhudhuria mapokezi ya mwenge wa uhuru huku akiahidi kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa wasiohudhuria.
“Wasiwasi wa DC Tesha ni watu wachache kujitokeza kutokana na watu wengi kutokuwa na mwamko na mwenge kama zamani ndiyo maana ameamua kuita walimu ofisini kwake na kuwatisha,” ameeleza mwalimu mmoja huku akiomba jina lake lihifadhiwe.
DC Tesha alipotafutwa na mtandao huu ili kuzungumzia suala hilo ikiwemo vitisho dhidi ya walimu, simu yake ya mkononi iliita pasipo kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (SMS) hakuweza kujibu.
James John mwandishi wa vikao vya jiji la Mwanza akiwa katika gari la jiji asubuhi ya leo ametangaza kuwa mwenge huo utalala wilayani Nyamagana na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo na wananchi wakitakiwa kushiriki na kujitokeza kuimba wimbo wa uhuru wa Tanzania.
Mkurungenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, kufuatia gari la Jiji kupita na kuwatangazia wananchi kusitisha shughuli zao, simu yake haikupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (SMS) hakujibu.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )