Bodi
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inapenda kuwatahadharisha
waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2016/2017 na umma
kwa imepokea taarifa kuwa kuna watu wasio waaminifu ambao si watumishi
wa Bodi huwapigia simu baadhi ya waombaji kwa lengo la kuwatapeli.
Taarifa
hizo za kitapeli zimekuwa zikisambazwa katika siku za hivi karibuni
kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii zikiwataka baadhi ya waombaji wa
mikopo au wadhamini wao kutuma fedha (Tshs 39,000/-) kwa namba ya simu
0716463190 ili fomu zao za maombi ya mikopo zilizowasilishwa Bodi
zirekebishwe kwa kuwa zimeonekana zina makosa na hivyo hawatapata
mikopo.
Namba
inayotumika kusambaza taarifa hiyo au kupiga simu kutoa taarifa hizo ni
0764640325 na mtu anayepiga anajitambulisha kwa jina la Charles Amos.
Bodi
ya Mikopo inapenda kuwataarifu wadau wake wote, wakiwemo wale walioomba
mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2016/2017 kuwa taarifa hizo
si za kweli. Mtu huyo ni tapeli na si mtumishi wa Bodi ya Mikopo.
Iwapo waombaji watapigiwa simu na matapeli hao, watoe taarifa kwa vyombo vya dola kwa hatua zaidi.
Aidha,
Bodi ya Mikopo inapenda kuwataarifu waombaji wa mikopo kuwa utaratibu
wa Bodi kuwasiliana na waombaji wa mikopo ambao fomu zao za maombi
hubainika kuwa na upungufu haujabadilika. Mara baada ya kazi ya ukaguzi
wa fomu kukamilika, Bodi ya Mikopo itatoa taarifa kupitia vyombo
mbalimbali vya habari, ikiwemo tovuti yake (www.heslb.go.tz) na kuwaalika waombaji kufanya marekebisho.
Taarifa hii pia inapatikana katika tovuti ya Bodi iliyotajwa hapo juu.
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA HABARI, ELIMU NA MAWASILIANO,
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU,
IJUMAA, AGOSTI 12, 2016
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )