Siku
moja baada ya Rais John Magufuli kuzuia usafirishaji wa mchanga wa
madini kwenda kuuchenjua nje ya nchi akitaka shughuli hizo zifanyike
nchini, imeelezwa kuwa utekelezaji wa dhamira hiyo utachukua muda mrefu
kutokana na mchakato wake.
Juzi,
Rais Magufuli alinukuliwa na vyombo vya habari wilayani Kahama akisema
katika uongozi wake hataki kuona mchanga huo ukisafirishwa.
Alisema
katika nchi zote zenye madini, Tanzania ndiyo pekee inayosafirisha
mchanga kwenda nje hivyo akaagiza shughuli hiyo ifanyike nchini.
Agizo
hilo limekuja wakati utafiti juu ya uwezekano wa Tanzania kuwekeza
katika mtambo wa kuchenjua mchanga wa dhahabu ya uliofanywa na Wakala wa
Ukaguzi Madini Tanzania (TMAA) Februari 2011, ukionyesha kuwa ni
uwekezaji unaohitaji fedha nyingi.
Ripoti
hiyo ilisema gharama za usimikaji mtambo kamili wenye uwezo wa
kuchenjua wastani wa tani 150,000 kwa mwaka, ingeweza kufikia Dola za
Marekani 500 milioni hadi Dola 800 milioni (sawa na Sh1.1 trilioni hadi
Sh1.74 trilioni za sasa).
Ripoti
hiyo ambayo ilikuwa na lengo la kuangalia uwezekano wa kuchenjua
mchanga unaosafirishwa na kampuni ya Acacia inayomiliki migodi ya
dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu, ilieleza kuwa baadhi ya mataifa
yanayosafirisha mchanga huo kwenda Japani na China ni Chile, Indonesia,
Peru, Marekani, Australia na Canada.
Kwa
mujibu wa ripoti hiyo, mgodi wa Barrick (sasa Accacia) huzalisha na
kusafirisha kati ya tani 25,000 na 50,000 za mchanga huo kwa mwaka ili
kuchuja kiwango cha madini yaliyomo.
Akitoa
maoni yake binafsi kuhusu agizo hilo, Makamu wa Rais wa Acacia, Deo
Mwanyika alisema msimamo wa Rais Magufuli ni sahihi lakini utekelezaji
wake utahitaji maandalizi kutokana na ukubwa wa gharama za uwekezaji wa
mtambo huo.
Huku
akisisitiza kuwa maoni hayo ni yake binafsi, Mwanyika alisema ipo haja
ya Serikali na sekta binafsi kukaa pamoja kwa ajili ya kujadili shughuli
za uwekezaji huo hapa nchini.
“Nimemsikiliza
Rais na nimemwelewa dhamira yake lakini hajamaanisha amezuia rasmi,
haiwezekani kuzuia ghafla shughuli hizo. Pia sisi (wazalishaji) ni
tofauti kabisa na sekta hiyo ya uchenjuaji, kwa hiyo itabidi kujadili
nani awekeze, upatikanaji wa mikopo itakuwaje na mambo mengi
yanayohusiana,” alisema.
Serikali
iliwahi kulieleza Bunge wakati ikijibu swali la aliyekuwa Mbunge wa
Kahama, James Lembeli, Aprili 2007 kuwa suala hilo ni la kisera kwa kuwa
wawekezaji wameruhusiwa na Serikali ilikwishajitoa kwenye biashara.
Akijibu
swali hilo ambalo Lembeli alitaka kujua kwa nini mtambo huo usijengwe
nchini, aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Lawrence Masha
alisema hali hiyo imetokana na Serikali kukosa wawekezaji au wawekezaji
kuchelewa kufanya hivyo hapa nchini.
Masha
alilishauri Bunge lishirikiane na Serikali kuendelea kuwakaribisha na
kuwashawishi wawekezaji kuja kuwekeza katika mtambo huo wa kuchenjua
mchanga, akibainisha kuwa uwekezaji huo unahitaji mtaji mkubwa.
Miaka
kadhaa iliyopita, aliyekuwa Mkurugenzi wa Ukaguzi, Uzalishaji na
Biashara ya Madini wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA),
Liberatus Chizuzu alikaririwa akisema kuwa gharama za uwekezaji wa
mtambo huo ni kubwa ikilinganishwa na thamani ya mapato yanayopatikana
kupitia uchenjuaji wa madini yaliyopo.
Chizuzu
alisema miongoni mwa masharti ya uwekezaji wa mtambo huo ni upatikanaji
wa umeme wa uhakika, jambo ambalo ni changamoto hapa nchini.
Angalizo la Lisu
Juzi,
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alitoa angalizo kuhusu hatua
hiyo ya Rais akisema Kwa kuzingatia kwamba wawekezaji hao wanalindwa
kisheria na kimkataba.
Mwanasheria
huyo mkuu wa Chadema alisema kwa mujibu wa Sheria ya Madini na Mikataba
ya Uendelezaji Madini (MDA), madini yote yanayochimbwa ni mali ya
wawekezaji.
Alisema
kwa kuzingatia kwamba wawekezaji hao wanalindwa kisheria na kimkataba,
hatua hiyo inaweza kuwafanya wawekezaji hao kwenda mahakama za
usuluhishi za kimataifa.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )