Waziri
wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amewataka makamanda wa polisi wa mikoa
kujitathmini kama wanatosha katika nafasi hizo, vinginevyo wajiandae
kuziachia.
Lugola
alitoa kauli hiyo jana alipofanya ziara ya kushtukiza katika kituo
kikuu cha polisi jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine alisema
baadhi ya makamanda hawajaanza kutekeleza maagizo yake kwa madai kuwa
yamekuwa yakitolewa kisiasa zaidi.
“Wakuu
wote wa vyombo vya ulinzi na usalama ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (Nida) wawe mguu sawa, maana hawajui siku wala
saa nitakapoibuka kwenye vituo na mikoa yao ili kuangalia maagizo yangu
kama yanatekelezwa au la, wengi wataondoka na kuwapisha wenye weledi na
uwezo wa kufanya kazi,” alisema Lugola.
Alisema
atamuandikia barua Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro
kuhusiana na maagizo anayoyatoa kwamba lazima yatekelezwe na makamanda
wa mikoa, lakini atakayeshindwa atalazimika kuwapisha wenzake.
Waziri
Lugola alirudia kauli yake kuhusu makosa yenye dhamana kwamba lazima
watu wapewe dhamana iwe sikukuu, usiku au siku za mwishoni mwa wiki na
kuwa Mtanzania yeyote ana haki ya kumwekea dhamana mtuhumiwa.
“Inspekta
Jenerali wa Polisi namuelekeza kwamba kila raia wa nchi hii awe
mfugaji, mvuvi, mkulima au mfanyabiashara anayo haki ya kumdhamini
Mtanzania mwenzake,” alisema.
Lugola
alisema, “Kinachotakiwa ni kutimiza vigezo vya huyo anayemdhamini kama
anafahamika, anatambulika na ataweza kumleta huyo aliyemdhamini kwenye
kituo cha polisi siku ambayo ameelekezwa kwenye hati yake ya dhamana.”
Akizungumza
katika ziara hiyo, kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto
aliahidi kuzifanyia kazi dosari zilizojitokeza ikiwemo ya kutotolewa
dhamana kwa watu wanaostahili, kukosekana kwa taarifa za watuhumiwa na
kukosekana kwa kibali cha kuhalalisha kuuzwa kwa pikipiki zilizokamatwa
na kukosekana wamiliki wake.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )