Vigogo
waliojilimbikizia mashamba makubwa ya mkonge wako hatarini kupokwa
kutokana na mpango wa serikali kuyafanyia ukaguzi wa kuwabaini
walioyatelekeza bila kuyaendeleza.
Mpango
huo umetangazwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
William Lukuvi, akisema serikali itaanza kufanya ukaguzi mashamba yote
ya mkonge nchini kwa lengo la kubaini yale ambayo hayafanyi vizuri ili
wayafute na kupatiwa watu wengine watakaokuwa na uwezo wa kuyaendeleza.
Aidha,
Lukuvi ameijia juu Bodi ya Mkonge Tanzania kwa kushindwa kusimamia
vizuri kampuni zinazozalizasha zao hilo ambapo mengi yao uendeshaji wake
hauna tija kwa kuwa hayatoi ajira za kutosha kwa wananchi wanaozunguka
eneo husika sambamba na kuikosesha serikali mapato.
Lukuvi
alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na uongozi wa kampuni ya
kuzalisha mkonge ya LM Investments Ltd iliyopo katika kijiji cha Ndungu
Wilaya ya Same Mkoa wa Kilimanjaro wakati akikamilisha ziara yake ya
kushughulikia migogoro ya ardhi katika wilaya za Hai, Moshi na Same.
“Mashamba
mengi ya mkonge hapa nchini uendelezaji wake hauna tija, hauridhishi na
wamiliki wake wanahodhi tu maeneo jambo linaloikosesha serikali mapato,
huku wengine wakitumia mashamba hayo kukopea fedha katika benki,”
alisema Lukuvi.
Alisema
pamoja na kuwapo Bodi ya Mkonge ambayo ina jukumu la kusimamia
uendeshaji zao hilo, lakini imeshindwa kufanya kazi ipasavyo, hivyo
kusababisha makapuni ya kuzalisha mkonge kufanya yanavyotaka.
“Kama
bodi ya Mkonge wameshindwa kuchukua hatua kwa wale wasiofanya vizuri
katika uzalishaji wa mkonge, basi sisi kama Wizara ya Ardhi tutafanya
ukaguzi kwa mashamba yote ya mkonge ili tubaini wale wasiofanya vizuri
na tuwanyang’anye na tuwapatie watu wengine wenye uwezo,” alisema
Lukuvi.
Kauli
ya Lukuvi inafuatia kutoridhishwa na uendeshaji wa Shamba la Mkonge la
Ndungu lenye ukubwa wa hekta 1,230 linalomilikiwa na Kampuni ya LM
Investments Ltd.
Shamba
hilo limekuwa na mgogoro na wananchi wa vijiji vitatu vya Ndungu, Gonja
Mperani na Msufini. Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni
ya LM Investments Ltd, Allan Chellangwa, shamba hilo limekuwa
likizalisha wastani wa tani 30 mpaka 50 kwa mwezi na lengo ni kuzalisha
tani 50 kwa mwezi huku wafanyakazi 24 wakiwa wameajiriwa.
Maelezo
hayo yalimshtua Lukuvi ambaye alisema uwiano wa hekta 1,230 na ajira za
watu 24 hauendani na kueleza kuwa lengo la serikali kutoa mashamba
makubwa kwa wawekezaji ni kutoa ajira kwa wananchi sambamba na kupata
mapato kupitia kodi na kusisitiza serikali haiwezi kuacha shamba lenye
ukubwa huo kutoa ajira za watu wachache tu.
Wenyeviti
wa vijiji vya Msufini, Gonja Mperani na Ndungu waliiomba serikali
kuwapatia ekari 100 kila kijiji ili ziwasaidie katika shughuli zao.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Msufini, Omar Mganga, alimueleza Lukuvi kuwa
kijiji chake kimekuwa na uhaba wa ardhi jambo linalosababisha wananchi
wa eneo hilo kukosa maeneo ya makazi na ya kuzikia.
Akizungumza
na wananchi wa vijiji vyote vitatu, Lukuvi aliwaeleza kuwa moja ya kazi
ya serikali ni kuondoa kero, kulinda wawekezaji na kutetea wanyonge na
kufafanua kuwa jukumu la serikali siyo kufukuza wawekezaji, ila ni
kutaka kuwa na wawekezaji wenye tija, watakaoleta teknolojia mpya pamoja
na kuongeza pato la taifa.
Katika
kutatua mgogoro huo, Lukuvi aliamuru vijiji hivyo vitatu vipatiwe jumla
ya hekta 300 kutoka hekta zinazomilikiwa LM Investments Ltd 1,230
ambapo hekta 71 ni zile zilizoongezwa tofauti na makubaliano ya
umilikishwaji mwaka 1998 na nyingine zitatoka ndani hekta zinazomilikiwa
na kampuni ambapo kila kijiji sasa kitapatiwa hekta 100 jambo
lililopokelewa kwa furaha na wananchi wa vijiji hivyo.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )