Watu
watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Wilayani Ilemela kwa tuhuma za
kujiunganishia umeme kinyemela kwenye nyumba zao kinyume na utaratibu
uliowekwa na TANESCO.
Taarifa
ya jeshi la polisi mkoa wa Mwanza imesema kuwa mnamo tarehe 31.07.2016
majira ya saa 5:10 asubuhi katika maeneo ya Ilemela Mlimani wilaya ya
Ilemela jiji na mkoa wa Mwanza, watu watatu wanashikiliwa na jeshi la
polisi kwa tuhuma za kujiunganishia umeme kinyemela kwenye nyumba zao
kinyume na sheria na utaratibu uliowekwa na TANESCO.
Imewataja
watu hao kuwa ni Boniphace Masamaki miaka 47, Lina Cosmas miaka 26 na
Ali Mohamed miaka 30 wote wakazi wa mtaa wa Ilemela Mlimani.
Aidha
watuhumiwa hao waliweza kukamatwa baada ya kupatikana kwa taarifa
kutoka kwa raia wema, ndipo jeshi la polisi kwa kushirikiana na maofisa
wa TANESCO waliweza kufanya msako maeneo hayo na kufanikiwa kuwakamata
watuhumiwa hao.
Watuhumiwa
wote wapo katika mahojiano na jeshi la polisi wakishirikiana na
TANESCO, pindi uchunguzi ukikamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.
Msako wa kuwasaka watu wengine ambao wamejiunganishia umeme kinyume na utaratibu bado unaendelea.
Kamanda
Wa Polisi Mkoa Wa Mwanza Naibu Kamishina Wa Polisi Ahmed Msangi anatoa
wito kwa wakazi wa jiji na mkoa wa Mwanza akiwataka kuacha tabia ya
kujiwekea umeme kinyemela katika nyumba zao kwani ni kosa la jinai
lakini pia wanahatarisha maisha ya familia pamoja na mali zao.
Amesema
jeshi la polisi kwa kushirikiana na wananchi wema na maofisa wa TANESCO
litahakikisha linawasaka na kuwatia nguvuni watu wote wanaodaiwa
kujiwekea umeme kinyemela kwenye nyumba zao na kuwafikisha kwenye vyombo
vya sheria.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )