WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amekataa kupokea msaada wa madawati uliotolewa na
Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) baada ya kubaini yametengenezwa chini ya
kiwango.
“Ofisa
Elimu njoo kagua haya madawati yaliyo mazuri nitayapokea na yaliyobaki
yarudishwe karakana yakatengenezwe upya huu si wakati wa kupokea vitu
vibovu,“ amesema.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Agosti 02, 2016) wakati
alipowasili katika kiwanja cha Mabau, Mtibwa kwa ajili ya kuzungumza na
wananchi ambapo alikabidhiwa madawati hayo na Meneja wa TFS….
Alisema
anatambua dhamira ya TFS ya kuunga mkono jitihada za Serikali za
kumaliza tatizo la upungufu wa madawati lakini hawezi kupokea kupokea
madawati yaliyotengenezwa chini ya kiwango.
Baada
ya Ofisa Elimu (Msingi) wa Wilaya ya Mvomero, Michael Ligola kukagua
madawati 102 yaliyoletwa uwanjani hapo madawati 84 yalibainika kuwa ni
mabovu na 14 tu ndiyo yalikuwa mazima.
Waziri
Mkuu alisema hawezi kupokea madawati hayo yaliyotolewa na Meneja wa
Msitu wa Mtibwa, Hamza Kateti na kuuagiza uongozi wa wilaya ufuatilie
suala hilo kwa kuwa walitakiwa kuyakagua kabla ya yeye kukabidhiwa.
Katika
hatua nyingine aliwasisitiza wazazi na walezi wa wilaya hiyo
kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shule na atakayeshindwa atachukuliwa
hatua kali za kisheria.
“Serikali
imewapunguzia mzigo kwa kuwaondolea michango na ada hivyo tumieni fursa
hiyo kwa kuwapeleka shule watoto wote waliofikia umri wa kwenda shule
na wasimamie masomo yao,” alisema.
Awali
mbunge wa jimbo la Mvomero, Saddiq Murad alisema miongoni mwa
changamoto kubwa inayoikabili wilaya hiyo ni pamoja na wafugaji kuingiza
mifugo katika mashamba hivyo amemuomba Waziri Mkuu kuingilia kati suala
hilo.
Akizungumzia
namna Serikali ilivyojipanga kutatua changamoto ya migogoro baina ya
wafugaji na wakulima Waziri Mkuu alisema wafugaji wenye mifugo mingi
watahamishiwa katika vitalu vinavyomilikiwa na ranchi za Taifa na wenye
mifugo michache watatengewa maeneo katika vijiji.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )