Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
amemaliza ziara yake ya siku NNE mkoani Mtwara kwa kuwahakikishia mamia
ya wakazi wa wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara kuwa serikali imetenga
zaidi ya bilioni 170 kwa ajili ya utekeleza wa mradi mkubwa wa maji
katika wilaya hiyo ili kuondoa tatizo la uhaba wa maji kwa wananchi wa
Tandahimba.
Makamu
wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti
wakati akihutubia mkutano wa hadhara mjini Tandahimba na wakati
amesimamishwa njiani na wananchi wa vijiji vya Kitama I na Kitama II
ambao walitaka kumsalimia akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani
Tandahimba mkoani Mtwara.
Makamu
wa Rais amesema mkakati wa serikali wa sasa unalenga kuhakikisha
wananchi wa Tandahimba na wa maeneo mengine nchini wanapata maji safi na
salama hali ambayo itaondoa usumbufu wa wananchi kutumia muda mwingi
kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za maendeleo.
Amesema
anaimani kubwa kuwa mradi huo wa maji utakapokamilika wilayani
Tandahimba mkoani Mtwara utakuwa ni suluhu ya kudumu ya uhaba wa maji
kwa wananchi hao wa Tandahimba.
Kuhusu
usafirishaji wa korosho kwa njia ya magendo, Makamu wa Rais Samia
Suluhu Hassan ameonya kuwa serikali kamwe haiwezi kuwavumilia watu
wanaofanya vitendo hivyo na watakaobainika watachukuliwa hatua kali za
kisheria ili kukomesha tabia hiyo.
Makamu
wa Rais amesema kuwa biashara ya magendo ya korosho inainyima serikali
mapato mengi ambayo yangesaidia shughuli za maendeleo za wananchi hivyo
ameuagiza uongozi wa mkoa wa Mtwara uchukue hatua za kukomesha biashara
hiyo haramu ambavyo ameifananisha na uhujumu uchumi kwa serikali.
Kuhusu
ubovu wa barabara kutoka mjini Mtwara hadi wilaya ya Tandahimba, Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema
serikali itajenga kilomita 50 za awali kwa kiwango cha lami katika
barabara hiyo ili kuimarisha shughuli za usafiri na usafirishaji kati ya
Mtwara mjini na wilaya ya Tandahimba.
Makamu
wa Rais pia ameuagiza uongozi wa mkoa wa Mtwara kukutana haraka na
Watendaji wa Wakala wa Barabara wa mkoa wa Mtwara ili kujadiliana kuhusu
namna gani ujenzi huo utakavyotekelezwa.
Akiwa
mjini Tandahimba, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameshiriki katika
zoezi la utoaji wa zawadi mbalimbali kwa uongozi wa shule ya sekondari
ya Tandahimba kwa kuingia katika shule 10 bora kitaifa katika matokeo ya
Kidato cha Sita ambapo Kampuni ya Startimes imetoa hundi ya shilingi
milioni Mbili kwajili ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wilayani humo.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Mtwara.
10-Sep-2016
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )