Aliyekuwa
mgombea urais wa Chadema akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, anajiandaa kuweka wazi
ushiriki wa aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba katika
mchakato wake wa kuhamia Chadema mpaka kuwa mgombea urais.
Akizungumza
kwa simu na mwandishi wa habari hii akiwa Nairobi nchini Kenya jana,
Lowassa ambaye pia alikuwa Waziri Mkuu, wakati wa Serikali ya Awamu ya
Nne ya Rais Jakaya Kikwete, alisema akirudi kutoka safari hiyo,
atafafanua mbele ya vyombo vya habari, tuhuma dhidi yake zilizotolewa na
Profesa Lipumba.
“Kwa
sasa naomba uniache kwanza maana nipo safarini Nairobi, nikija Dar es
Salaam nitazungumzia suala hilo kwa undani kupitia vyombo vya habari,
hivyo subirini nirudi,” alisema Lowassa.
Madai ya Lipumba
Hivi
karibuni Profesa Lipumba alitupa lawama moja kwa moja kwa Lowassa,
kwamba ujio wake ndani ya Ukawa, unaoundwa na Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi
na NLD, ndiyo ulisababisha matatizo katika vyama hivyo kwa kiasi
kikubwa.
Kwa
mujibu wa Profesa Lipumba, kabla ya kujiunga kwa Lowassa Ukawa, vyama
hivyo walikaa kikao ambacho aliwashauri viongozi wenzake wa Ukawa
kutazama mtu anayeweza kuendana na mahitaji yao awe ndani au nje ya
umoja huo.
Alisema
ni kweli aliona wangeweza kupata ushindi kupitia Lowassa, lakini hata
ushindi huo ungepatikana, wangeenda kusimamia mambo gani? Maana suala ni
kusimamia katika eneo fulani.
Alifafanua
kuwa suala lililopo katika siasa ni baada ya kuchaguliwa, uunde
serikali ili usimamie misingi fulani ambayo itakidhi mahitaji ya
wananchi.
“Sisi
tulisema tunahitaji serikali inayowajibika, itakayopambana na rushwa,
itakayotumia rasilimali za nchi vizuri, na itakayohakikisha mali ya
asili ya Tanzania inawasaidia Watanzania wote,” alisema na kuongeza kuwa hayo Lowassa asingeweza.
Baada
ya kikao hicho cha kumjadili Lowassa, Profesa Lipumba alisema walifanya
kingine wakiwa na Mbowe (Freeman, Mwenyekiti wa Chadema); Mbatia
(James, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi) na Lowassa kujadili suala hilo kwa
mara ya pili kuwa ni vyema CUF, wakaribishwe kwanza ambapo walikuwa
hatua za mwisho.
Alisema
baada ya mchakato huo kwisha, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif
Hamad, alianza vikao vingine visivyomshirikisha yeye Lipumba, kwa
kumwalika Mbowe ili wafanye mazungumzo.
Lipumba
alidai kuwa Mbowe alipoitwa na Maalim Seif kwenda Zanzibar, alimfuata
na kumweleza kuwa ameitwa na Makamu wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar.
“Mbowe
alinipigia simu akaniambia kuwa ameitwa kwenye kikao na kwamba ndio
kulikuwa na hoja ya Lowassa kuingia Ukawa, wakati Chadema walikuwa na
msimamo kuwa kwenye Ukawa asikaribishwe mtu wa nje,”alifafanua.
Alisema
Mbowe aliendelea kumweleza kuwa, baada ya kikao kile ndipo Chadema
waligundua kuwa kuna sintofahamu ndani ya CUF, jambo lililowafanya wao
Chadema watoe hoja ya kuwa na mgombea wao, kwakuwa watakuwa na wabunge
wengi basi hata Waziri Mkuu atatoka huko na CUF itatoa mgombea mwenza.
Lipumba
alisema baada ya hali hiyo kutokea; ya Maalim Seif kufanya vikao
vingine bila kumshirikisha, alikuwa katika wakati mgumu maana hata
mazungumzo yale hakushirikishwa, ilihali yeye ndio Mwenyekiti wa CUF na
yalikuwa yanafanywa na Katibu kimnya kimnya.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )