Siku
tatu baada ya kutuliza vurugu baina ya viongozi na wanachama wa Jumuiya
ya Vijana ya CCM (UVCCM), polisi inamshikilia mwenyekiti wa umoja huo,
Lengai Ole Sabaya kwa tuhuma za kughushi kitambulisho cha Idara ya
Usalama wa Taifa.
Viongozi
hao walipambana Alhamisi wiki hii wakati wakigombea ofisi ya umoja huo
ya mkoa, vurugu zinazodaiwa kusababishwa na mgogoro wa chini kwa chini
uliodumu kwa miezi miwili kati ya makundi mawili yanayokinzana.
Wakati hali hiyo haijatulia, juzi saa 6.00 usiku, Sabaya alikamatwa katika baa ya Mile Stone akiwa na wenzake.
Habari
zilizopatikana jijini Arusha zinasema kitambulisho hicho kilipelekwa
kituo kikuu cha polisi ambako kulifunguliwa jadala la kesi ya madai
namba RB 5055/2016. Ilifunguliwa na hoteli ya Sky Way aliyokwenda kulala
na kuondoka bila kulipa gharama za malazi.
Awali,
ilidaiwa kwamba mwenyekiti huyo aliweka rehani kitambulisho hicho na
simu yake ili kupewa muda wa kulipa deni la hoteli hiyo.
Meneja wa hoteli hiyo, Filipo John alisema kiongozi huyo alikuwa akidaiwa Sh309,400 za siku sita alizolala hotelini hapo.
Pia,
John alikiri kupokea kitambulisho hicho na simu ambavyo alisema baada
ya kiongozi huyo kuondoka bila kulipa, alipeleka malalamiko kwa uongozi
wa mtaa na baadaye alipeleka kesi hiyo polisi.
“Nilipeleka
kesi kwa balozi na mwenyekiti wa mtaa, lakini walishauri vitu vyake
vipelekwe polisi. Baada ya kunilipa nilifuta kesi,” alisema meneja huyo.
Kamanda
wa polisi wa Mkoa, Charles Mkumbo alisema wanaendelea kumshikilia Ole
Sabaya kwa ajili ya upelelezi na atafikishwa mahakamani kesho.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )