Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi, imetupilia mbali pingamizi
lililowekwa na mawakili wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), katika kesi
iliyofunguliwa na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema).
Awali,
mawakili wa NHC walidai kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza
shauri hilo na kwamba mkataba baina ya Mbowe na NHC juu ya umiliki wa
jengo la Bilcanas lililopo mtaa wa Makunganya jijini Dar es Salaam
umeisha.
Upande
wa utetezi ukiongozwa na wakili Peter kibatala ulidai kuwa, mahakama
hiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, hivyo inaweza ikatoa uamuzi
wowote na ndiyo maana wamewasilisha maombi hayo ili yatolewe uamuzi.
Akitoa
uamuzi wa pingamizi la mawakili wa NHC jana, baada ya kuwa amesikiliza
hoja za mawakili wa pande zote mbili, Jaji Siyovelwa Mwangasi alisema
kuwa hoja za Mawakili wa NHC hazina mashiko kisheria kwani suala la
mkataba wa umiliki Jengo hilo linahitaji ushahidi.
Jaji
Mwangasi alisisitiza kuwa zuio la NHC kutopiga mnada mali za Mbowe,
lilizozichukua wiki mbili zilizopita kupitia mawakala wa kampuni ya
Fosters Auctioneers katika ukumbi wa Bilcanas na katika ofisi za kampuni
ya Free Media lipo pale pele.
Shirika
hilo linamtuhumu Mbowe kutolipa deni la Sh. 1.3 bilioni, ikiwa ni jumla
ya fedha za kodi ya kupangishwa kwenye jengo hilo huku Mbowe akifungua
kesi katika Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi, kupinga madai hayo ya NHC.
Katika
kesi hiyo namba 722 ya mwaka 2016, Mbowe anawakilishwa na Mawakili na
Peter Kibatala na Omary Msemo ilihali NHC ikiwakilishwa na mawakili wake
Aloyce Sekule na Miriam Mungula.
Katika
hoja zake Mbowe anadai kuwa, yeye na shirika hilo walikubaliana kwamba
alikarabati na kulipanua jengo hilo kwa gharama zake kwa asilimia 100,
makubaliano ambayo waliyaingia mwaka 1997.
Katika
makubaliano hayo, Mbowe amedai kuwa walikubaliana kumiliki jengo hilo
kwa pamoja kwa muda wa miaka 99, huku yeye akitakiwa kupata asilimia 75
katika mgawanyo wa mapato na NHC ikitakiwa kupata asilimia 25.
Hivyo
amedai kuwa hatua ya NHC kumtoa kwenye jengo na kuchukua mali zake ni
kuvunja mkataba huo. Mbowe aliondolewa kwenye jengo hilo mnamo Septemba
Mosi mwaka huu.
Baada
ya mahakama kufanyia uamuzi pingamizi lililowekwa na mawakili wa NHC,
kesi hiyo imeahirishwa mpaka tarehe 27 Septemba, mwaka huu ambapo
itaanza kusikilizwa rasmi.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )