Mbwana Samatta katika moja ya matukio awapo uwanjani.
BAADA ya kuanza vibaya hatua ya makundi ya Europa League kwa kufungwa
mabao 3-2 na wenyeji Rapid Viena katika mchezo wa Kundi F Alhamisi
Uwanja wa Allianz, Viena, Austria, mshambuliaji wa Tanzania, Mbwana Ally
Samatta na timu yake, KRC Genk leo wanarejea kwenye Ligi ya Ubelgiji.Samatta na Genk yake leo watakuwa wenyeji wa Anderlecht Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji, wakitoka kufungwa mechi mbili mfululizo, ukiwemo wa Jumapili iliyopita walipofungwa 2-0 na Standard Liege katika Ligi ya Ubelgiji pia.
Samatta amecheza mechi mbili mfululizo bila kufunga bao, kwani Alhamisi mabao ya Genk yalifungwa na Leon Bailey yote, la kwanza dakika ya 29 na la pili dakika ya 90 kwa penalty, huku ya wenyeji, Rapid Viena yakifungwa na Stefan Schwab dakika ya 51, Joelinton Cassio Apolinario de Lira maarufu tu kama Joelinton dakika ya 59 na Omar Colley aliyejifunga dakika ya 60.
Tangu amejiunga na Genk Januari mwaka huu kutoka TP Mazembe ya DRC, Samatta amecheza jumla ya mechi 25 za mashindano yote, 18 msimu uliopita na saba msimu huu, akifunga mabao nane, matatu msimu huu na matano msimu uliopita.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )