Featured
Loading...

Simulizi: Msamaha Wa Mama- 02


Msamaha
MWANDISHI/MTUNZI Saed Bin Salim
Machozi yalishaanza kunitoka, mama naye tayari alikuwa anabubujikwa na machozi kwa nilichomuambia.
“Mama yangu mimi nateseka sana mwanao, naomba uniambie kuhusu baba niteseke kwa kuchekwa kuishi na mama yangu lakini nikiwa tayari nimeujua ukweli wote, wapi aliko baba yangu?
Nikienda shule mimi natukanwa mama, mara naambiwa hivi mara vile, unasikia raha gani hasa mwanao ninavyofanyiwa vitendo kama hivyo? najisikia vibaya mama yangu nambie ukweli niujue, kikubwa kipi hasa unanificha?
Niliongea nikiwa nabubujikwa machozi. Sikuamini juu ya sauti ya huruma niliyoitumia kuongea na mama kama mama angeshindwa kunambia ukweli, hatimaye alitoka alikokuwa amesimama na kuingia ndani.
Ukweli niliumia sana kwa kitendo cha mama, nilimgeukia akiwa tayari amenipa mgongo nikajaribu kumuita bila kuitika, alipoingia ndani maneno ya hasira nilijikuta yakinitoka bila kujali kama ananisikia au laa!
“Najua unafurahi sana ninavyoteseka, hunipendi mama hunipendi, unanifanya niishi kama mnyama wakati ni binadam kama wengine kwa nini lakini? au na wewe sio mama yangu uliniokota?
Nilikunja miguu yangu na kuiweka mikono juu nikainamisha uso na kuendelea kulia.
Mama baada ya kuingia ndani alipanda moja kwa moja hadi kitandani, aliendelea kulia kwa uchungu kutokana na kitu ninachomuuliza kila siku kumuuma, sikufahamu kwa nini haitaji kuniambia ukweli, nilikuwa mtu wa kulalamika kila leo ili aniambie, nilijaribu kumrubuni kwa kutumia akili zangu za utoto japo anambie tu baba yangu yuko wapi lakini bado sikufanikiwa.
Alikuwa mtu mwenye huruma sana, Kwa nilivyomzoea sikuitaji kuamini kama ni roho ya mama yangu huyu huyu anayekubali mwanae nilie kila siku kisa baba, alinijengea mazingira ya kuamini uenda kuna siri nzito sana anaificha nisiifahamu, ila nilijipa moyo wa kuamini ipo siku nitaujua ukweli hata kama nitachelewa, na kilichokuwa kinanipa imani ni methali tunazosoma kila siku shule, huku Nikiapa kwa Mungu kama nikiujua ukweli na ukawa uko tofauti nitatokea kumchukia sana mama yangu japo namuona kila siku akihangaika pekee juu yangu.
Baada ya kulia kwa muda mrefu niliingia ndani nikamkuta mama yupo kitandani akiwa bado ana uwekundu wa macho, nilijua moja kwa moja amelia sana ilibidi nimsogelee na kumuomba anisamehe, nilimpenda sana lakini ni hasira tu ambazo zilikuwa zikinipelekea nimuulize kuhusu baba kila leo japo nilikuwa najua kabisa nikimuambia suala hilo anachukia hata kama alikuwa anacheka.
“Nisamehe sana mama ni hasira tu ambazo huwa zinaniingia mpaka kukuuliza jambo hilo ambalo najua linakukera kila leo. Nilisema kwa upole.
alinishika kichwani huku machozi yakimtoka upya.
“Nimekusamehe mwanangu.”
Tabasam la machozi liliingia usoni mwangu, nilimuangalia mama nikamshika machoni kumfuta machozi yaliyokuwa yanamtoka. Aliniangalia kwa huzuni machozi yakiwa bado yanamlenga, nilipogonganisha macho yangu na yake nikajua kuna kitu atakuwa ananisikitikia na kunionea huruma sana.
“Ngoja niende jikoni nikuandalie chakula si unaona usiku huu unaingia? Aliongea akiwa anainuka kitandani mama.
“ndiyo mama.”
“sawa, basi mimi naingia jikoni chukua vitabu usome usome hapa, giza likiingia utawasha kibatali nikimaliza kupika ule ulale kesho uwahi shule sawa baba!
“kesho jumamosi.” Nilimjibu.
“Eh nilisahau kabisaaa! kumbe kesho uko nyumbani.
“ndiyo
“bado si mbaya, mtoto kulala mapema ni wajibu wake, nikimaliza kupika utakula ulale kesho tuamkie shambani sawa baba.
“Sawa mama.”
Aliinuka na kusogea sehemu vilipokuwa vyombo, alichukua sufuria mbili, kiberiti pamoja na mfuniko kuelekea nje kulikokuwa na jiko.
Kipindi anataka kutoka nilimuita.
“Mama naomba unirushia huo mkoba wangu wa shule.
aliangalia sehemu ulipo mkoba, akanirushia na kwenda nje kwa ajili ya kupika.
*********
Mama huyu aliejulikana kwa jina la Bi       Najma baada ya kuingia jikoni na kuanza kupika, dimbwi zito la mawazo lilimshika ghafla kipindi amekaa pembeni ya mafiga, alishika shavu lake na kujiuliza vitu ambavyo majibu yake yalikuwa ni magumu sana kwa wakati ule lakini pia ni mepesi kwake kuyajibu, Kijana Seid aliendelea kujisomea ndani akisubiri chakula kiive, japo alikuwa mdogo lakini aliamini elimu ndiyo msingi wa maisha na ndiyo kitu pekee cha kumuondoa kwenye umasikini walionao yeye na mama yake.
“Sijui mwanangu anafikiria nini mpaka kuniuliza kuhusu baba yake kila siku, laiti kama angekuwa anajua yaliyonikuta na uchungu ninaousikia, asingeniuliza kuhusu huyu mwanaume, mmmh ila ipo siku nitamwambia ukweli kwa sababu ni haki yake, Eh Mungu nisaidie, sina nia ya kumficha mwanangu namuonea huruma tu mtoto mdogo anataka kujua mambo makubwa na mazito. Alijisemea moyoni.
Aliendelea kuwa na mawazo mpaka chakula kilipoiva, alikitoa jikoni akazima jiko na kuingia ndani akiwa na sufuria mikononi.
**********
Niligeuka nikaangalia mlangoni baada ya kusikia mlango ukifunguliwa.
“Bado unasoma mwanangu? Aliniuliza akiwa anaweka sufuria chini.
“Ndiyo mama, ushamaliza? Nlimjibu na kumtupia swali.
“bado kula tu hapa, nakuwekea chakula kwenye sahani kipoe mimi naenda kuoga, endelea kusoma nikirudi kitakuwa kishapoa ule utandike ulale sawa!
“Sawa nimekuelewa.
“Au unataka nikutandikie? Aliniuliza swali lililonifanya nitabasamu.
“ Hapana mama nitatandika tu mwenyewe. Lakini mama maji hamna unaenda kuoga nini?
nilimuuliza nilipokumbuka vidumu nimeviacha bombani.
“Itabidi nioge haya haya ya kunywa nitafanyaje sasa, wewe si umeacha vidumu bombani?
Nilikaa kimya sikuwa na la kuongezea, alimimina maji yaliyokuwa kwenye ndoo ya maji ya kunywa na kwenda kwenye bafu lililopo hatua 20 hivi kutoka kwenye nyumba yetu kwa ajili ya kuoga.
Giza tayari lilishaingia, nilishusha kanga iliyokuwa kwenye dirisha kama pazia ambayo ipo mpaka leo kuzuia mbuu wasiingie ndani, nilichukua kibatali nikawasha, nilikisogeza karibu na daftari langu nililokuwa nasoma, nikaendelea kupitia baadhi ya maswali na majibu kujijenga vizuri kiakili.
Somo nililokuwa nikipenda tokea niko darasa la kwanza ni Hisabati, nilikuwa tayari kufeli masomo mengine lakini si somo hili, nilihakikisha napata mia chini ya mia kila mtihani unaokuja mbele yangu wa hesabu, hata walimu waliokuwa wakinifundisha hesabu walifahamu wazi kuwa nalipenda na kufanya juu chini wakinikazania kuhakikisha sifeli. Alamu zangu kubwa zilikuwa ni tisini mpaka mia. Walimu wote shuleni walinipenda kutokana na adabu, heshima na mwenendo mzuri wa masomo yangu darasani.
Namshukuru sana Mungu wangu na mama yangu pia aliekuwa kipau mbele kuhakikisha nakuwa vizuri masomoni, alikuwa yuko tayari kufanya lolote kuhakikisha pesa yoyote iliyotakiwa shuleni inapatikana, akili nlizokuwa nazionesha pamoja na jitihada aliamini nitafika ngazi za juu katika masomo.
Japo nilikuwa darasa la tatu tu lakini walimu wote walinipenda kuanzia usafi na kwa mengine mengi niliyokuwa nayo ambayo mwalimu kama mwalimu anapenda kuona kwa mwanafunzi.
Mama alitoka bafuni na kunikuta nikiwa bado najisomea, alisogea pembeni yangu akanangalia nami niliinua uso wangu nikaachia tabasam baada ya kumkuta mama amenitazama.
“Mbona unaniangalia mama? nilimuuliza
“Hapana mwanangu, nioneshe mlipo soma leo.”
Nilifunua madaftari tuliosoma siku hiyo nikamuonesha, alifurahi sana alipokuta vema vema masomo yote matatu, alipomaliza kukagua alianza kunifundisha hesabu za mbele kama ilivyokuwa kawaida yake,
Pesa za kunipeleka tution hakuwa nazo, hivyo yeye aliamua kuwa mwalimu wangu wa nyumbani hasa katika masomo mawili hesabu na kiswahili, kupitia yeye nilipata mwangaza mkubwa sana darasani na kuonekana bora kila mara kutokana na kukifanyia mazoezi kitu cha mbele kupitia mama.
Ilipofika saa mbili kamili, mama aliniomba nifunike madaftari nikale kisha nilale, nilifanya hivyo madaftari yangu yote nikayaweka kwenye mkoba, niliinuka na kwenda kutundika mkoba wangu kwenye kimsumari kilichokuwa mlangoni, nikachukua chakula kilichokuwa juu ya ndoo na kuanza kula.
“Mama wewe huli? nilimuuliza baada ya kumuangalia na kumuona hana mpango wa kula.”
“Nakula mwanangu, we kula ulale sawa baba.”
Sikuongea tena kwa sababu kiazi kilikuwa mdomoni, sekunde kadhaa zilipita nkamuangalia tena, nlivyomuona ni kama mtu ambae alikuwa yuko mbali sana kimawazo.
“Mbona unaonekana una mawazo? Ilinibidi nimuulize swali hilo, aliniangalia na kunambia sina mawazo ya aina yoyote mwanangu maliza kula ukalale….”
******
Najma aliendelea kumuangalia mwanae Seid, alitingisha kichwa akimsikitikia baada ya kukumbuka mengi mazito kwenye kichwa chake kuhusu mwanae.
“Masikini mwanangu anaonekana ana akili sana, nakuomba mungu umuongoze apate kile kilichomo akilini mwake na cha ziada, nami naomba unisaidie nipate riziki zangu kwa njia nzuri nimsomeshe mwanangu huenda ndiyo msaada wangu mkubwa. Mhh maisha haya!!! Baba mtu yuko mjini anakula vyakula vizuri, analalia kitanda kizuri, mwanae analalia vyakula vigumu kama hivi kwa nini wanaume wako hivi? Japo angekuja basi kumchukua mwanaye akaishi nae huko kwa sababu ana maisha mazuri, mimi aniache na shida zangu nilizonazo.”
Aliwaza kichwani mwake jicho likigonga usoni mwa seid wakati yuko bize na kula.
*****
Kutokana na mapenzi ya mama aliyonayo kwangu, alipanga zamu ya kulala kitandani kwa wiki moja moja.
Usikose kufuatilia sehemu ya tatu ya mkasa huu Msamaha wa Mama kesho saa mbili kamili asubuhi bila kukosa!

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top