Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia Kamati yake ya Maudhui
imekifungia kituo cha Redio 5 Arusha kwa kipindi cha miezi mitatu pamoja
na kukitoza faini ya sh. Milioni 5 kwa kosa la kukiuka baadhi ya Kanuni
za Huduma za Utangazaji (maudhui) kupitia kipindi chake cha Matukio
kilichorushwa Agosti 25, 2016.
Kwa
mujibu wa taarifa ya kamati hiyo, katika kipindi hicho Mbunge wa Jimbo
la Arusha Mjini Mh. Godbless Lema alitamka maneno ya kashfa yaliyolenga
kumdhslilisha Rais John Magufuli na serikali kwa ujumla.
Wakati
akisoma maamuzi ya kamati hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui
Joseph Mapunda, aliongeza kuwa kituo hicho pia kilirusha maneno yaliyo
tamkwa na Lema ambayo yalikuwa yakihamasisha wananchi kushiriki katika
maandamano ya Ukuta yaliyopigwa marufuku na Jeshi la Polisi.
“Maneno
ya Lema yalilenga kuhamasisha wananchi kupambana na jeshi la polisi na
hivyo kusababisha uvunjifu wa amani na kuhatarisha usalama wa Taifa,” alisema.
Mapunda
alisema uamuzi huo umetolewa na kamati hiyo baada ya kamati hiyo
kusikiliza maelezo ya utetezi yaliyotolewa na wa Uongozi wa Redio 5
Arusha.
“Baada
ya kusikiliza maelezo ya utetezi kamati imeridhia kuwa kipindi cha
matukio kilikiuka baadhi ya kanuni za maudhui namba 5(a,b,c,d,f,h) 6(2)
(b, c) na 18 (1) (b),” alisema.
Aliongeza kuwa ”
kituo hicho kinatozwa faini ya sh. Milioni 5 ambazo zitatakiwa kulipwa
ndani ya siku 30 kuanzia leo, kinafungiwa kwa miezi 3 na kuwekwa chini
ya uangalizi maalumu kwa muda wa Mwaka 1 baada ya kipindi cha kufungiwa
kumalizika, “
Hata hivyo, Mapunda alisema haki ya wahusika kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo iko wazi ndani ya siku 30 kuanzia leo.
Kwa
upande wa kituo cha redio cha Magic Fm ambacho nacho pia kwa mujibu wa
kamati hiyo kinadaiwa kukiuka kanuni za maudhui kupitia kipindi chake
cha Morning Magic kipengele cha Paka Rangi ambapo kilirusha maneno
yanayodaiwa kumkejeli rais na wananchi, kimepewa onyo kali pamoja na
kutakiwa kuomba radhi kwa muda wa siku tatu mfululizo.
“Baada
ya kusikiliza na kutafakari kwa kina maelezo ya utetezi yaliyotolewa na
Uongozi wa Magic Fm Redio, Kamati ya Maudhui imeridhika kuwa kipindi
cha Morning Magic kilikiuka baadhi ya kanuni za huduma za utangazaji
2005. Kamati ya maudhui inaamua kutoa onyo kali kwa Magic Radio, ” alisema na kuongeza.
“Pia
inatakiwa kumuomba radhi Rais John Magufuli, wasikilizaji na wananchi
kwa ujumla. Tangazo la kuomba radhi litolewe kwa siku tatu mfululizo
katika taarifa za habari za saa 10.00 alasriri, na 3.00 usiku kuanzia
tarehe 17,9,2016.”
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )