Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kutafuta fedha za
mafunzo kwa ajili ya wahadhiri wa vyuo vikuu nchini ili kuziba pengo la
wahadhiri waandamizi lililopo hivi sasa
Waziri Mkuu pia amevitaka vyuo hivyo viweke utaratibu wa kuachiana nafasi ama kurithishana kazi (succession plan).
Amesema
yeye binafsi anatambua upungufu uliopo umesababishwa na masharti ya
ajira za mkataba kwa wahadhiri waandamizi kuwa miaka 65 na maprofesa
kuwa miaka 70.
Ametoa
kauli hiyo leo (Jumanne, Oktoba 25, 2016) wakati akifunga kilele cha
maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyoanza jana
kwenye ukumbi wa Nkrumah. Kampasi ya Mwalimu J. K. Nyerere, jijini Dar
es Salaam.
“Ninatambua
kuwa katika vyuo vya umma kuna upungufu mkubwa wa wahadhiri waandamizi
na maprofesa na hivyo kuathiri hali ya utoaji wa taaluma kwa fani za
‘Post-Graduates’. Ninajua kuwa pamoja na sababu nyingine, hali hii
inachangiwa pia na masharti ya ajira za mikataba kwa wahadhiri
waandamizi kuwa miaka 65 na maprofesa kuwa miaka 70.,” amesema.
Akizungumzia
kuhusu maslahi ya watumishi wa vyuo hivyo, kikiwemo Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam, Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria
kuhakikisha inaondoa malimbikizo ya madai kwa watumishi wote wa umma na
hivi sasa inakamilisha uhakiki wa taarifa za kiutumishi kwa watumishi wa
umma ili kubaini watumishi hewa.
“Hadi
kufikia tarehe 20 Oktoba, 2016 zoezi linaloendelea hivi sasa,
limesaidia kuwabaini watumishi wa umma hewa wapatao 16,500. Baada ya
zoezi hilo, tutarudia uhakiki wa madeni yote yaliyowasilishwa Serikalini
na kisha tutalipa madeni ya watumishi wote,” amesema.
Akifafanua
kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Waziri Mkuu amesema
Serikali inaendelea kufanya uhakiki wa taarifa za waombaji wa mikopo.
Ametoa wito kwa wanufaika na waombaji wote wa mikopo wahakikishe kuwa
wanatoa taarifa zilizo sahihi na za uhakika.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali ilikwishaongeza bajeti ya mikopo ya
elimu ya juu kutoka sh. bilioni 340 mwaka 2015/2016 hadi sh. bilioni
483 kwa mwaka 2016/2017.
Mapema,
akielezea utendaji kazi wa chuo hicho katika miaka yote 55, Makamu Mkuu
wa Chuo hicho, Prof. Rwekaza Mukandala amesema chuo hicho kinakabliwa
na changamoto ya uhaba wa wanataaluma waandamizi wa fani mbalimbali.
“Chimbuko
la changamoto hii ni kusitishwa kwa ajira katika taasisi za umma kwenye
miaka ya 1990. Kutoajiriwa kwa wanataaluma chipukizi kwa miaka mingi,
kulivuruga utaratibu wa miaka mingi wa kurithishana uzoefu baina ya
wanataaluma wanaostaafu na wale ambao wangelichukua nafasi zao,”
amesema.
“Hali
hii iko kwenye vyuo vikongwe ambako mamia ya wanataaluma wazoefu
wanastaafu kwa wakati mmoja na wengi wa wanataaluma walioajiriwa hivi
karibuni bado wako masomoni au wangali chipukizi katika taaluma zao na
hivyo hawana uwezo wa kutosha kubeba majukumu ya kufundisha katika ngazi
za digrii za umahiri na uzamivu,” amesema.
Wakati
huohuo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,
Dkt. Leonard Akwilapo alisema wizara hiyo imetenga kiasi cha sh. bilioni
9 kwa ajili ya kufanya ukarabati wa miundombinu kwenye chuo hicho
zikiwemo maabara.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )