
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba.
Ibrahim Mussa, Dar es SalaamKUFUATIA mwamuzi wa kati Martin Saanya kushindwa kumudu kuchezesha mechi ya watani wa jadi kati ya Yanga na Simba, uongozi wa Simba umeamua kumshutumu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kutokana na kitendo cha kufurahia mwajiri wake kuruhusu bao la mkono katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Mchezo huo ulipigwa juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar na kuchezeshwa na mwamuzi huyo mwenye beji ya Fifa ambaye pia ni muajiriwa wa Jeshi la Magereza mkoani Morogoro.

Wachezaji wa Simba wakishangilia.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara
alisema kuwa wameamua kutoa malalamiko yao kwa waziri huyo kwa madai ya
kusahau majukumu yake na kugeuka kiongozi wa Yanga kutokana na kitendo
kilichofanywa na mwamuzi wa mchezo huo ambaye yupo chini yake.“Klabu inatoa malalamiko yake kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe Mwigulu Nchemba, bila shaka amesahau majukumu yake ya kazi na kugeuka kiongozi wa Yanga. Tunajua ni haki yake kuwa na mapenzi kwa klabu aliyoichagua lakini vitendo vyake anavyovifanya vinaacha maswali mengi kuliko majibu ukizingatia nafasi yake kama waziri mwenye dhamana ya kuongoza wizara nyeti.
“Itakumbukwa majuzi waziri huyu alifanya ziara mkoani Morogoro kuzungumza na vikosi anavyoviongoza na inajulikana pia mwamuzi wa mchezo wa jana (juzi) Martin Saanya ni mwajiriwa wa Jeshi la Magereza mkoani Morogoro, wote tulishuhudia Mwigulu alishangilia bao la hovyo la mwajiriwa wake Saanya.”
Manara aliongeza: “Pia waziri huyu alitoa kauli tata kuwa angetamani siku moja mashabiki wa klabu inayoshangilia wapinzani wa Yanga wakipigwa mabomu ya machozi na Askari wa Jeshi la Polisi, tunajiuliza yale mabomu ya jana pale Uwanja wa Taifa ndio utekelezaji wa maagizo ya bosi Mwigulu?
“Lakini pia matumizi ya rasilimali za umma yakiwemo magari ya serikali katika shughuli za mara kwa mara za Yanga napo kunaacha maswali mengi mno, sasa Wanasimba wanauliza kila waziri anayeshabikia Simba akiwemo Waziri Mkuu akifanya vitendo hivi kutakuwa na utawala gani serikalini? Imani yetu viongozi wakuu wa nchi watamuonya, vinginevyo atatengeneza chuki baina ya mashabiki wa Simba dhidi ya serikali yao.”
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )