Akizungumza na Bongo5 wiki hii, Katibu Mkuu wa Baraza la Sanaa Taifa (BASATA), Godfrey Mngereza amesema amesikia kuna bifu kati ya Diamond Platnumz na Ali Kiba lakini hawajapokea taarifa rasmi ambayo inaonyesha mmoja kati yao akilalamika kuhusu mwenzie.
“Kwa upande wa serikali au BASATA tunafanya kazi kwa kuzingatia maandishi au taarifa rasmi, kwahiyo suala kuwepo kwa kutokuelewana kati ya Ali Kiba na Diamond halijatufikia rasmi,” alisema Mngereza. “Huu ni ushabiki au mashabiki ndio wanaleta haya, kwa hiyo ni ushabiki wa team hii na hii na tunaliona. Lakini kwa kuwa halijaja rasmi likija rasmi tutalishughulikia,” aliendelea kuongeza Katibu huyo.
Aidha alisema, “Lakini tukikutana na wao wenyewe wapo safi, kwa hiyo wanaosababisha hivyo ni mashabiki kwa sababu hata wachezaji wa Simba na Yanga wale ni wachezaji wapo kwenye tasnia moja, ni marafiki wanakaa pamoja, wanakula pamoja ni kama wanamichezo wa ngumi, wewe ukiwa nje unaangalia wao wanapigana kweli lakini ule ni mchezo. Kwahiyo mimi hii naona ni ushabiki wa mashabiki ambapo kimsingi huwezi kuwazua. Pia ni kwa sababu hakuna aliyelalamika, kimsingi sisi ni walezi wa wasanii mmoja angelalamika sisi tungeuwita upande mwingine,”
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )