Featured
Loading...

Walichoongea Rais Magufuli na Rais Museveni nchini Uganda


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wamewaagiza Mawaziri wa nchi hizi mbili kujadiliana juu ya namna ya kuongeza biashara kati ya nchi hizi ili kupata manufaa makubwa zaidi ya uhusiano na ushirikiano wa kidugu uliopo.

Viongozi hao wametoa kauli hiyo jana tarehe 10 Novemba, 2017 baada ya kufanya mazungumzo rasmi na kisha kuzungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ndogo ya Masaka nchini Uganda ambako Mhe. Rais Magufuli ameendelea na ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku 3.

Akisisitiza juu ya agizo hilo Mhe. Rais Magufuli amesema kwa muda mrefu biashara kati ya Tanzania na Uganda imekuwa ni takribani shilingi Bilioni 200 kwa mwaka kiasi ambacho ni kidogo mno ikilinganishwa na fursa zilizopo, uhusiano na ushirikiano wa kidugu uliojengwa tangu enzi za Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

“Tumewaagiza Mawaziri na wataalamu wakae na waangalie vikwazo vyote vinavyosababisha tufanye biashara kwa kiasi kidogo, wakishajadili watatuambia tufanye nini, tunataka kuona biashara ya Tanzania na Uganda inakua, hivi sasa Uganda imewekeza Dola za Marekani Milioni 47 tu nchini Tanzania na kuzalisha ajira 146,000, kiasi hiki ni kidogo sana, ni lazima tuongeze” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kuhusu hatua ambazo Tanzania imeanza kuchukua Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma umbali wa kilometa 726, Serikali imekarabati reli iliyopo, pamoja na kivuko cha mabehewa ya treni cha Umoja katika ziwa Victoria ili kuwezesha mizigo ya kutoka bandari ya Dar es Salaam kufika Kampala kwa gharama nafuu na pia inaendelea kujenga na kuimarisha barabara za mpakani.

“Napenda pia kukushukuru Mhe. Rais Museveni kwamba Serikali yako sasa itajenga kipande cha kilometa 11 za reli kutoka Portbell hadi Kampala, na sisi tumeamua kuweka bandari kavu pale Mwanza ili wafanyabiashara wa Uganda wasisumbuke kwenda hadi Dar es Salaam, mizigo yao wataipata Mwanza, hii ni njia ya uhakika na nafuu ya kusafirisha mizigo” ameongeza Mhe. Rais Magufuli.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari Mhe. Rais Magufuli ameeleza kuwa Tanzania imejipanga kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Uganda kwa kuhakikisha miradi mbalimbali inakwenda vizuri ikiwemo kituo cha pamoja cha huduma za mpakani (One Stop Border Post – OSBP) na mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Kwa upande wake Mhe. Rais Museveni amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi kubwa anazozifanya kupambana na rushwa na kuimarisha uchumi, na amemuagiza Waziri wake wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Monica Azuba Ntege kuharakisha mchakato wa ujenzi wa kipande cha reli cha kilometa 11 kutoka bandari ya Portbell hadi Kampala ili usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli kutoka bandari Dar es Salaam uanze mara moja.

Mhe. Rais Museveni amesisitiza kukuzwa kwa biashara katika ya Tanzania na Uganda hasa wakati huu ambapo Uganda inahitaji kununua gesi ya Tanzania kwa ajili ya viwanda vyake vya mbolea na chuma na pia kurudisha historia ambapo Uganda ilikuwa mnunuzi mkubwa wa bidhaa za Tanzania.

Kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari Marais wote wawili wameshuhudua utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Shirika la Utangazaji wa Uganda (UBC) na makubaliano kati ya Jeshi la Polisi la Tanzania na Jeshi la Polisi la Uganda.

Mhe. Rais Magufuli atamaliza ziara yake rasmi ya siku 3 kesho na kurejea nchini Tanzania.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Masaka, Uganda

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top