Kufuatia
vuguvugu la hivi karibuni la wanasiasa kuhama vyama vyao na kuhamia
Chama cha Mapinduzi (CCM) huku wengine wakitoka CCM na kuhamia upinzani,
Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe
ameamua kutoa ya moyoni kuhusiana na sarakasi hizo za kisiasa.
Katika
chama chake cha ACT-Wazalendo, Zitto amepoteza wanasiasa kama Samson
Mwigamba, Dkt. Kitila Mkumbo na wanachama wengine 10 ambao wametimkia
CCM huku aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Mama Anna Elisha Mghwira
akijiuzulu nafasi hiyo na kusalia kuwa mwanachama wa kawaida baada ya
kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Zitto ameandika yafuatayo;
“Kuhama
au kubadili Chama cha Siasa sio jambo geni katika siasa zetu, na ni
haki ya kikatiba ya Mtanzania yoyote kufanya ivyo. Kitu cha msingi ni
kitendo hicho kuongozwa na imani thabiti kwenye misingi ya chama
unachokwenda.
Siku
zote ninaamini kuwa vyama vinapaswa kujengwa juu ya misingi ya Itikadi.
Sisi ACT Wazalendo itikadi yetu imejengwa kwenye Azimio la Tabora
kuhusu Siasa ya Ujamaa wa Kidemokrasia. Tutaendelea kufanya siasa za
masuala na kuimarisha mfumo wa Vyama vingi nchini kwetu.
Mimi
Binafsi na Wanachama wenzangu wa ACT wazalendo tunawatakia heri na
mafanikio wenzetu waliojiunga na vyama vingine. Sisi wengine tutaendelea
kujenga Vyama kama Taasisi muhimu za Maendeleo katika Nchi yetu. Kamwe
hatuwezi kuruhusu nchi yetu kuwa ya chama kimoja. Kwa mazingira ya
kisiasa ya sasa, kuwa mwanachama wa Chama cha Upinzani ni uzalendo
uliotukuka.
Ni
dhahiri kuwa Chama kuondokewa na wanachama wake sio jambo jema. Lakini
ukitazama watu wanaohama vyama ni wanasiasa wale wale wa siku zote na
walikuwa kwenye vyama vingine kabla na kuhamia vyama wanavyotoka sasa.
Kwangu mimi kuna somo moja kubwa nalo ni kuandaa aina Mpya ya wanasiasa,
wanasiasa wanaojengwa kwenye itikadi na misingi. Kazi kubwa iliyopo
mbele yangu kama Kiongozi ni kuandaa kizazi kipya cha Viongozi wa
kisiasa wajamaa. Hiyo ndio kazi ninayofanya sasa. Forward Ever, Backward
Never.”
Zitto Kabwe, Mb
Mtwara
23/11/2017.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )