Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za
kuuawa kwa askari 14 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
waliopo katika operesheni ya ulinzi wa amani katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Pamoja na askari hao kuuawa, askari wengine 44 wamejeruhiwa na 2 hawajulikani walipo.
Kufuatia
vifo hivyo Mhe. Dkt. Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance Salvatory Mabeyo, Maafisa na Askari wa
wote JWTZ, familia za marehemu na Watanzania wote kwa kuwapoteza
mashujaa waliokuwa wakitekeleza wajibu wao.
“Nimeshtushwa
na kusikitishwa sana na vifo vya vijana wetu, askari shupavu na
mashujaa waliopoteza maisha wakiwa katika majukumu ya kulinda amani kwa
majirani zetu DRC” amesema Mhe. Dkt. Magufuli.
Amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, Amina.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania wote kuwa watulivu na kuwa na
subira wakati Serikali ikiendelea kuchukua hatua zinazostahili baada ya
kutokea tukio hilo, na pia amewaombea majeruhi wote wapone haraka ili
waweze kuendelea na majukumu yao ya kawaida.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino, Dodoma
08 Desemba, 2017
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )