Kufuatia
zoezi la serikali la kupanua na kuboresha miundo mbinu mbalimbali
nchini hususan ya barabara katika jiji la Dar es Salaam ambapo imelazimu
baadhi ya maeneo kubomolewa ili kupisha zoezi hilo la upanuzi, Kanisa
la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima nalo limekumbwa na kadhia
ya kubomolewa.
Kanisa
hilo lililoko jirani kabisa na Barabara ya Morogoro ambayo serikali
imepanga kuipanua ili kurahisisha usafiri na kupunguza foleni,
lilitakiwa kubomolewa kutokana na kuwa ndani ya eneo la hifadhi ya
barabara hiyo.
Mchungaji
Biyagaza wa Kanisa la Ufufuo na Uzima lililoko chini ya Askofu Gwajima,
ameeleza kuwa serikali iliwapatia notisi ya siku 30 ili wabomoe kipande
cha jengo la kanisa hilo kilichopo ndani ya eneo la hifadhi ya
barabara.
“Ni
kweli tunayo notice ya mwezi mmoja ya kuhakikisha kwamba eneo ambalo ni
hifadhi ya barabara tunaliacha. Na hifadhi ya barabara ni mita 90
kuanzia katikati. Bahati nzuri wale waliokuja kuweka alama zao
walipofika hapa na wahandisi , mafundi na baadhi ya watu wa kanisani
walikuwepo. Basi tukawaambia wapime mita 90 zinapoishia. Kwa hiyo
wakapima mita 90 zilipoishia wakaweka alama, wakasema basi nyie mnaweza
mkabomoa upande huu na upande huu mkauacha kwa ajili ya hifadhi ya
barabara,” alisema Mchungaji Biyagaza.
“Sisi
baada ya hapo tukaona tujipange kwa ajili kuachia eneo la barabara ili
shughuli nyingine ambazo ni mpango wa maendeleo ya serikali ziweze
kuendelea na sisi tuweze kuendelea na eneo letu vizuri. Kwa hivyo kile
kipande chote ambacho ni cha barabara na tukaongeza ndani kidogo chote
tumekiondoa. Na hili eneo linalobaki tunapaimarisha ili nyumba ya Bwana
iweze kufanya kazi yake ya kutoa huduma za kiroho,” aliongeza.
Mchungaji
Biyagaza alieleza japokuwa eneo la jengo limepungua, eneo lililobakia
linaimarishwa ili kanisa hilo liweze kuendelea kutoa huduma za kiroho
kwa waumini wake.
Aidha
kufuatia zoezi hilo la upanuzi wa barabara ya Morogoro ambalo linaenda
sambamba na ujenzi wa barabara za juu (fly-over) katika makutano ya
barabara eneo la Ubungo, umepelekea kubomolewa kwa majengo mbalimbali
ikiwemo majengo ya wizara ya Maji na Umwagiliaji pamoja na jengo la
Makao Makuu ya Shirika la Umeme Tanzania ambayo yamebomolewa kufuatia
agizo la Rais Dkt. John pombe Magufuli.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )