Featured
Loading...

CUF ya Lipumba Yawaomba radhi wapiga kura Kinondoni Baada ya Mbunge wake Maulid Mtulia Kujiuzulu

Chama cha Wananchi  (CUF), upande wa Profesa  Ibrahim  Lipumba kimewaomba radhi wapiga kura wa jimbo la Kinondoni  baada ya aliyekuwa mbunge  wa jimbo hilo kupitia chama hicho, Maulid Mtulia kujiuzulu.

Kauli imetolewa  leo, Jumatatu  Desemba 4, 2017 na Mkurugenzi  wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma, Abdul  Kambaya wakati akizungumza  na wanahabari kwenye makao makuu ya chama hicho Buguruni.

Amesema CUF iliwaaminisha wakazi wa Kinondoni  kwa kumpeleka Mtulia kugombea jimbo hilo kwa kuwa ni mtu makini na mambo mengi alishaanza kuyatekeleza ikiwamo kuzuia bomoa bomoa lakini wanasikitika kujiuzulu kwake.

"CUF  haikutarajia kuingia katika uchaguzi mdogo hasa jimbo la Kinondoni  kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 labda kingetokea kifo. Tunawaomba radhi wakazi wa Kinondoni," amesema Kambaya.

Kambaya amesema sababu za kujiuzulu  alizozitoa Mtulia ni za msingi kwake lakini kwao hazina maana wala mashiko.

Desemba 2, Mtulia alitangaza kujiuzulu nafasi ya ubunge huku akisema amefikia uamuzi huo bila kushawishia na mtu yoyote na ameamua kuhamia CCM.

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top