Jeshi la polisi mkoani Mwanza linamshikilia mtu mmoja kwa kosa la kujifanya daktari, katika hospitali ya mkoa Sekou Toure.
Joseph
Mbagata 25,mkazi wa mtaa wa Mabatini jijini humo amekamatwa leo Desemba
18 na jeshi hilo baada ya kubainika kwamba sio mwanataaluma na alikuwa
akiwatapeli wagonjwa kwa kuwaomba hongo, kitendo ambacho ni kosa
kisheria.
Taarifa
kutoka kwa jeshi hilo zimesema kwamba mtuhumiwa alikuwa akiwaomba
hongo, huku akiahidi kuleta dawa muhimu na pia kufanya mipango ili
mgonjwa apate huduma kwa haraka.
Awali
zilipatikana taarifa kuwa siku chache zilizopita alionekana mtu
aliyevalia mavazi ya udaktari na kujifanya daktari, kisha anapita wodini
kuwaona wagonjwa. Pia ilisemekana kuwa mtu huyo tayari amechukua
Sh30,000 kwa mgonjwa ili aweze kumpatia matibabu.
Aidha
baada ya tuhuma hizo kufika katika uongozi wa hospitali waliweka mtego
na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa, akiwa amevalia mavazi ya udaktari
huku akiwa amesimama nje ya wodi ya upasuaji.
“Tumekuwa
tukilalamikiwa kwamba kuna baadhi ya madaktari hapa hawana ujuzi wala
hawajitambui, kumbe ni dhahiri kwamba hao watu wapo na kuanzia sasa
lazima tufanye ukaguzi wa hali ya juu ili hali hiyo isije ikajitokeza
tena maana ni sehemu ya kuhatarisha maisha,” amesema mmoja wa madakatri
katika hospitali hiyo ambaye hakutaka kutajwa majina.
Baada
ya daktari huyo feki kukamatwa, uongozi wa hospitali ulitoa taarifa
polisi, ambapo askari walifika eneo la tukio na kumuweka mtuhumiwa chini
ya ulinzi kisha kumfanyia upekuzi kwenye begi alilobeba na kukuta
mavazi yanayotumiwa na madaktari katika vyumba vya upasuaji.
Polisi
wapo katika upelelezi na mahojiano na mtuhumiwa pindi uchunguzi
ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani ili hatua stahiki za
kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake.
Kamanda
wa polisi mkoa wa Mwanza naibu kamishina wa polisi Ahmed Msangi ametoa
wito kwa wananchi hususani wagonjwa waliopo hospitalini akiwaomba kuwa
makini na watu ambao ni matapeli wa aina kama hiyo wenye nia ovu dhidi
yao.
Aidha
pia aliwaomba viongozi wa hospitali zote kuendelea kutoa taarifa kwa
polisi kuhusiana na watu wanao watilia shaka hospitalini, ili waweze
kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )