Featured
Loading...

Majaliwa aizungumzia Dar es salaam itakavyobaki Baada ya Serikali Kuhamia Dodoma

Serikali imesema kwamba kuhamia Dodoma haiondoi hadhi ya Jiji la Dar es Salaam, na kwamba mji huo utabaki kuwa sehemu ya biashara.

Hayo yamesemwa leo na Waziri  Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati akifungua  ofisi  ya Shirika la maendeleo ya Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa kuwepo kwa ofisi ya Umoja wa Mataifa mkoani Dodoma ni ishara ya kukamilika kwa serikali kuhamia rasmi mkoani humo.

"Leo nafungua ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa hapa Dodoma, zaidi ya watumishi 2376 wameshahamia Dodoma, mimi tayari nimehamia mapema, Makamu wa Rais Samia Suluhu ataungana nasi mwishoni mwa mwezi huu , mwakani tunategemea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli atahamia huku", amesema Majaliwa.

Pia ameongeza kwa kusema, "Umoja wa Mataifa una mchango mkubwa sana katika Taifa letu, imechangia mipango mingi ya maendeleo , mpango wa kwanza ulianza mwaka 2011, wakati huu wa pili umeanza 2016 na utaishia 2021".

Aidha Majaliwa amesema hadhi ya mkoa wa Dar es salaam haitopungua ila itakuwa sehemu rasmi ya biashara.

"Viongozi kuhamia Dodoma hakuharibu hadhi ya mkoa huo, utabakia kuwa ni sehemu sahihi ya biashara, tunatengeneza njia sita ambazo zitatoka Ubungo hadi  Chalinze, tunaimarisha mwendokasi ufike maeneo mengi pamoja na njia za reli iendayo haraka" , ameongeza Majaliwa.

Mpango wa kuhamia Dodoma ulianzishwa na aliyekuwa Baba wa Taifa  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1973, utekelezaji umeanza kufanyika mwaka 2017 ndani ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli.

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top