Wakazi
wa mji wa Dodoma na viunga vyake mapema leo Jumamosi, Desemba 9, 2017
wamejitokeza kushuhudia maadhimisho ya miaka 56 ya uhuru kwenye Uwanja
wa Jamhuri.
Taratibu za ukaguzi wa kiusalama, zilifanya misururu mirefu baada ya kutumika geti moja kuingilia ndani ya Uwanja wa Jamuhuri.
Hali hiyo ilifanya misururu mrefu kuanzia geti la kuingilia uwanjani kufika katika barabara inayoelekea Nkuhungu.
Mabasi makubwa yanayotoka katika wilaya za jirani yalionekana yakishusha watu tangu saa 11.00 alfajiri kuwahi foleni.
Watu walianza kuingia uwanjani huku vikundi mbalimbali vya burudani vikitumbuiza.
Saa 2:00 asubuhi, gwaride maalumu lililojumuisha vikosi vya ulinzi na usalama viliingia uwanjani.
Viongozi
mbalimbali walianza kuwasili uwanjani kuanzia saa 1:00 asubuhi wakiwemo
mke wa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mama Fatma
Karume, mke wa Rais ya Kwanza wa Tanzania Mama Maria Nyerere na
aliyekuwa makamu wa kwanza wa Rais, Mohammed Gharib Bilal.
Mwenyekiti
wa CUF anayetambulika na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, Profesa
Ibrahim Lipumba na mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema ni baadhi ya
viongozi wa kisiasa walioonekana uwanjani hapo.
Viongozi
wengine waliofika asubuhi uwanjani hapo ni Rais wa Zanzibar, Ali
Mohamed Shein, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, mke wa Rais, Janeth
Magufuli, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa, majaji wakuu wa
makatibu wakuu wa wizara mbalimbali, Spika wa Bunge Job Ndugai, mawaziri
na wabunge.
Tayari Uwanja wa Jamhuri umejaa na wananchi wamezuiwa kuingia katika uwanja huo na milango yote imefungwa.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )