MSHAMBULIAJI wa
Simba, Jamal Mnyate, ameomba barua kwa uongozi wa timu hiyo
itakayomruhusu kuondoka na kwenda kwenye klabu nyingine kucheza soka.
Awali, kulikuwepo na taarifa za mshambuliaji huyo kuwepo kwenye orodha
ya wachezaji watakaoachwa kwenye usajili huu wa dirisha dogo
lililofunguliwa Novemba 15, mwaka huu.
Mchezaji mwingine anayetajwa kuachwa ni mshambuliaji Juma Liuzio ambaye yeye uongozi wa Simba umepanga kumtoa kwa mkopo.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Jumatatu limezipata, mshambuliaji
huyo anaomba barua hiyo ya kuachwa ili aende zake akaichezee Lipuli FC
inayonolewa na Selemani Matola.
Aliongeza kuwa, mshambuliaji huyo tayari amekutana na mabosi wake huku
akiahidiwa kupatiwa barua hiyo ya kuondoka Simba baada ya kukosa nafasi
ya kucheza.
“Mnyate hatutakuwa naye katika mzunguko wa pili wa ligi kuu, kwani yeye
mwenyewe ameomba barua ya kuachwa baada ya kuwepo taarifa za kutolewa
kwa mkopo.
“Hivyo, yeye mwenyewe ameomba aachwe moja kwa moja na siyo kwa mkopo
kama wanavyotaka wenyewe Simba na maamuzi hayo ameyatoa baada ya kuona
anakosa nafasi ya kucheza,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Kocha Mkuu wa Lipuli FC, Selemani Matola kuzungumzia hilo
juu ya mshambuliaji huyo kuomba aende huko, alisema: “Ni kweli kabisa
hizo taarifa, kama mambo yakienda vizuri basi Mnyate tutakuwa naye
katika mzunguko wa pili wa ligi kuu.
“Kwani yeye mwenyewe ameonyesha nia ya kuja kuichezea Lipuli, hivyo
ninamkaribisha na kama unavyojua timu yangu ina tatizo katika safu ya
ushambuliaji, ninaamini kama akija yeye basi timu itaimarika zaidi.”
Wilbert Molandi| Dar es Salaam
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )