Na Mathias Canal, Dodoma
Uongozi
wa Chuo cha Madini Dodoma kilichopewa ithibati kamili ya kutoa mafunzo
ya umahiri yaani Competence Based Education and Training System (CBET)
umetakiwa kujitathmini ikiwemo kutatua changamoto zinazokikabili chuo
hicho ndani ya wiki mbili.
Kauli
hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Mhe Dotto Mashaka
Biteko jana 15 Januari 2018 alipotembelea chuoni hapo na kujionea hali
ya ufanisi wa chuo hicho huku akikerwa na uduni wa utunzaji wa vifaa
katika chumba cha maabara ya uchenjuaji wa madini.
Mhe
Biteko alisema kuwa pamoja na changamoto lukuki walizoainisha katika
taarifa ya chuo iliyosomwa na Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Ndg Vincent
Willium Pazzia ikiwa ni pamoja na uchache wa bajeti, uhaba wa wakufunzi
katika fani za uhandisi na usimamizi wa mazingira migodini na upungufu
wa ofisi za watumishi, wanatakiwa kuwa na mikakati ya kukabiliana nazo
ndani ya wiki mbili zitakazofika ukomo mwishoni mwa mwezi huu.
Alisema
kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli haitatoa fedha mahali
ambapo hakuna matokeo ili ziliwe na watu wasiokuwa na matakwa mema na
Taifa.
Aliongeza
kuwa katika Wizara ya madini kumekuwa na malalmiko mengi kuliko
utendaji jambo ambalo lisipotafutiwa ufumbuzi wa kudumu haraka
litabakisha usugu na uvivu wa kufikiri kwa baadhi ya watendaji na
kusalia kufanya kazi kwa mazoea pasina kuwa na ubunifu.
Naibu
Waziri wa Madini Mhe Biteko alisema kuwa wakati Taifa likiwa linaelekea
kuwa katika uchumi wa kati na mapinduzi ya viwanda huku rasilimali za
madini zikipewa umuhimu mkubwa ni lazima watendaji wakubali kukabiliana
na changamoto mbalimbali kwani tiba ya changamoto hizo ni pamoja na
kuzikabili na kuzipatia ufumbuzi wa haraka.
Aidha,
ameutaka uongozi wa chuo hicho cha madini kuhakikisha kuwa kinazalisha
wataalamu wengi katika sekta ya madini ambao watalisaidia Taifa
kutekeleza majukumu muhimu ya serikali ikiwemo uzalendo na ulinzi wa
mali za umma.
Alisema
kuwa watendaji wote serikalini wanapaswa kutambua kuwa wana jukumu
kubwa moja la kuhakikisha kuwa wanatekeleza kwa ubora na umakini mkubwa
maelekezo rasmi ya serikali ambayo yamebainishwa katika ilani ya
uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi katika kipindi cha mwaka 2015-2020.
MWISHO
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )