Rais
John Magufuli amesema Rais Paul Kagame wa Rwanda anafaa kuongoza Umoja
wa Afrika (AU) kwa sababu ya historia yake na hivyo anazifahamu
changamoto zinazolikabili bara hili.
Rais
Magufuli alisema hayo jana Ikulu wakati Kagame alipofanya ziara ya
kikazi ya siku moja, ikiwa ni mara yake ya pili kufanya ziara tangu Rais
Magufuli alipoapishwa. Alifanya ziara kwa mara ya kwanza Julai Mosi,
2016.
Magufuli
alimwaga sifa hizo akianzia matatizo yaliyoibuka nchini Libya baada ya
kiongozi wake wa kijeshi, Muamar Gadaffi kuondolewa madarakani kwa
vurugu licha ya kuliongoza taifa hilo vizuri kiuchumi.
“Baada
ya kiongozi wa Libya kuondoka, na nyinyi nyote mnajua, matokeo yake ni
haya. Na haya ndiyo ya ukweli na utabaki kuwa ukweli,” alisema Rais
Magufuli katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jana.
“Nina
uhakika Mheshimiwa Kagame atakapokuwa mwenyekiti wetu Afrika,
atayaadress (atayashughulikia haya), atayaadress vizuri masuala ya
migogoro miongoni mwa nchi za Afrika, atayaaddress vizuri masuala ya
ukoloni mamboleo unaoweza kuletwa na mtu yeyote kutoka nje akasababisha
matatizo kwa Waafrika.
“Mheshimiwa
Kagame hadi kufikia urais anafahamu shida za wananchi wa Rwanda; anajua
historia ya Rwanda ilitokotoka hadi ikatokea genocide (mauaji ya watu
wengi). Anafahamu mateso ya Wanyarwanda; anafahamu mateso yanayoweza
kuletwa na mtu hata mmoja tu, inawezekana ikawa ni media kwa kutangaza
au kuandika kitu cha ovyo kikaleta multiplying effect.”
Alisema
ndio maana anaamini kutokana na mchango wake kwa Afrika na kwa sababu
ni mwanamapinduzi mzuri, uzoefu wake utasaidia maendeleo ya Afrika.
“Rais
Kagame ni mwanamapinduzi wa kweli wa Afrika, ameishi maisha ya
Kiafrika, maisha ya mateso tangu akiwa kijana; ameishi kwenye nchi za
ugenini kama mkimbizi, anayafahamu mateso ya kijana,” alisema.
“Kwa
hiyo kwa yale maisha aliyoyaishi kama mkimbizi, kama kijana, nina
uhakika ataleta mageuzi makubwa Rwanda ambayo ameshaanza kuyaleta,
lakini ataleta mageuzi makubwa Afrika.”
Alisema
Tanzania inamuunga mkono Rais Kagame kwa nguvu zote ili kuwepo kwa
mabadiliko ya kiuchumi kwa Waafrika wote hasa kwa vijana ambao ndiyo
nguvu kazi kubwa katika bara hili.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )