Featured
Loading...

Wizara Nne Zakutana Kushughulikia Changamoto Za Uwanja Wa Ndege JNIA

Na John Bukuku
SERIKALI kupitia wizara zake nne tofauti zimeamua kufanya jitihada za kuondoa changamoto ya  msongamano wa wageni wanaiongia na kutoka nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA) jijijini Dar es Salaam.

Pia kuondoa changamoto ya joto katika eneo la kuchukulia mizigo pamoja na kushughulikia hati za kusafiria kwa wageni wanaoingia nchini pamoja na changamoto ya ufinyu wa eneo la kusubiri huduma uwanjani.

Wizara hizo zimekutana jana katika uwanja huo na kufanya ziara ya kukagua shughuli za utoaji huduma kwa wageni na kubaini mambo kadhaa.

Mawaziri hao ni Wizara ya Maliasili na Utalii Dk.Hamis Kigwangala, Wizara ya Mambo ya Ndani Dk.Mwigulu Nchemba, Wizara ya Mambo ya Nje kupitia Naibu Waziri Dk.Susan Kolimba na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano Atashasta Nditiye.

Akizungumza uwanjani hapo baada ya kufanyika ziara hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Dk. Susan Kolimba alisema  wanaridhishwa na hatua zinazochukuliwa za kuondoa changamoto zinazoelezwa kuwepo katika uwanja huo.

 Alisema baada ya kufanya ziara na kuona namna ambavyo huduma zinatolewa kwa wageni mbalimbali wanaoingia nchini ameridhishwa na hatua ambazo zinachukuliwa ni hakika zitaondoa kero hizo haraka.

“Awali mgeni alikuwa anahudumiwa kwa saa tatu lakini hivi saa mgeni anahudumiwa kwa saa moja,”alisema Dk.Kolimba.

Kwa upande wa Waziri wa Mambo ya Ndani Dk.Mwigulu Nchemba alisema jitihada zinafanywa kutatua changamoto hizo na kuna matumaini makubwa ya kuzipatia ufumbuzi kwa haraka.

“Hatua ambazo wizara yetu inachukua ni kuharakisha utoaji huduma wa hati ya kusafiria kwa njia ya kieletroniki badala ya mfumo wa sasa na  siku za karibuni mchakato utakamilika.

“Pia wizara yetu itaongeza idadi ya madawati ya kutolea huduma kwa wageni ikiwa sambamba na kuongeza watoaji huduma uwanjani hapo,”alisema.

Alifafanua kuwa taarifa zinaonesha kwa sasa kuna unafuu mkubwa wa kutoa huduma kwani badala ya saa tatu ambazo zilikuwa zinatumia awali hivi sasa muda wa utoaji huduma umeshuka hadi saa moja.

“Mbali ya kuboresha huduma kwa nafasi yetu tutahakikisha pia tunaongeza ulinzi na usalama katika viwanja vyetu vyote nchini ili kudhibiti wageni wenye nia ovu na nchi yetu,”alisema.

Akizungumza changamoto zilizopo uwanjani hapo Waziri wa Maliasili na Utalii Dk.Kigwangala alisema wamefikia hatua hiyo baada ya baadhi ya wageni na hasa watalii wanaiongia nchini kulalamika.

Alitaja baadhi ya malalamiko ni kwamba wanatumia zaidi ya saa tatu kupata huduma wakiwa uwanjani hapo.Pia joto kali na ufinyu wa eneo katika eneo ambalo wageni wanasubiri kuhudumiwa.

Hivyo Dkt.Kigwangala alisema kutokana na malalamiko hayo na mengine kadhaa hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa na kueleza Agosti 8 mwaka 2017 manaibu waziri wa wizara hizo nne walikutana kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi.

Alisisitiza ukarimu kwa wageni ni muhimu katika maeneo mbalimbali ya utoaji huduma, akitoa mfano  kuwa hata polisi uwanjani hapo katika kutekeleza majukumu yao ni vema wakawa wakarimu licha ya kwamba wakati mwingine wamedaiwa kutumia nguvu.

 “Ni vema sasa wakawa na ukarimu ndani yake ili mgeni adhibitiwe kistaarabu kwa yule ambaye atakuwa ameshikiliwa kutokana na sababu yoyote akiwa uwanjani hapo”.

Alisema anatamani kuona kuanzia uwanja huo wa ndege hadi hotelini ambako mgeni anakwenda anatumia muda mchache, anapata nafasi ya kuona picha za viongozi mbalimbali ambazo zitakuwa uwanjani , picha za wanyama na video zinaonesha utalii wa Tanzania.

“Kumpokea mgeni jambo moja lakini namna ya kumhudumia ni jambo jingine na ndilo muhimu zaidi.Tunataka mgeni afurahie kuwa Tanzania,”amesema.

Wakati huo huo  Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Nditiye alisema wizara yao tayari imechukua hatua za kuondoa changamoto zilizopo ikiwamo ya kufunga viyoyozi(AC) kwa ajili ya kuondoa hali ya joto.

Alisema AC zilizopo ni za muda mrefu kwani ziliwekwa tangu majengo ya uwanja huo yalipojengwa.Pia unafanyika ukarabati wa kuongeza eneo kwa ajili ya wageni wanaosubiri kuhudumiwa.

Aliongeza kuna jitihada ambazo Serikali inafanya za kuondoa msongamano wa wageni ikiwamo ya kuharakisha ujenzi wa jengo jipya la kusafiria wageni la Terminal III litakalohudumia watu milioni sita badala ya jengo la sasa ambalo lengo lake lilikuwa kuhudumia watu milioni moja.

“Ujenzi wa jengo jipya umekamilika kwa asilimia 70 na litakapokuwa tayari kwa asilimia 100 litaanza kutumika kwani kasi ya ujenzi inakwenda vizuri,’alisema.

Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
© Copyright MZALENDO HURU
Back To Top