Wafanyakazi
watano wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc)
wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka
sita ya uhujumu uchumi, ikiwamo kula njama na kughushi saini ya Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari
Makamba.
Washtakiwa
hao wamesomewa mashtaka hayo jana Jumatano Oktoba 31, 2018 na wakili wa
Serikali, Faraja Nguka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina
Mmbando.
Akisoma
mashtaka hayo, Nguka alidai washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka
sita ikiwamo la kula njama, mawili ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya
uongo, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kusababisha hasara ya
Sh 160 milioni.
Wakati
washtakiwa hao wakisomewa mashtaka hayo, mshtakiwa mwenzao, ofisa
mazingira wa Nemc, Magori Wambura (38) ambaye hakuwepo mahakamani,
imetolewa hati ya kumkamata ili asomewe mashtaka yanayowakabili wenzake.
Washtakiwa
waliosomewa mashtaka ni ofisa mazingira wa Nemc, Deusdith Katwale (38)
mkazi wa Ubungo Msewe, mtaalam wa Tehama, Luciana Lawi (33) mkazi wa
Ubungo Msewe, sekretari wa baraza hilo, Edna Lutanjuka (51) mkazi wa
Mbezi Beach St Gasper, msaidizi wa ofisa Mwaruka Mwaruka (42) mkazi wa
Ukonga Mombasa na ofisa mazingira NEMC, Lilian Laizer (27) mkazi wa
Ukonga Mombasa.
Washtakiwa
hao kwa pamoja wanadaiwa kati ya Septemba 27, 2016 na April Mosi,
2018 Dar es Salaam walikula njama ya kutenda kosa la kughushi.
Katika
shtaka la pili washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Oktoba 17, 2017 Dar es
Salaam kwa udanganyifu walighushi cheti cha tathmini ya uharibifu wa
mazingira chenye namba ya usajili EC/EIA/3366 wakijaribu kuonyesha kuwa
cheti hicho ni halali na kwamba kimetolewa na Nemc wakati wakijua si
kweli.
Katika
shtaka la tatu wanadaiwa kuwa Oktoba, 2017 Dar es Salaam kwa nia ovu
walighushi saini ya Makamba katika cheti cha tathmini ya uharibifu wa
mazingira chenye usajili namba EC/ EIA/3366 wakijaribu kuonyesha kuwa
cheti hicho ni halali na kimetolewa na Nemc wakati wakijua si kweli.
Katika
shtaka la nne, mshtakiwa Edna anadaiwa kuwa Oktoba 2017 katika ofisi
za Nemc Makao Makuu Dar es Salaam kwa kujua alitoa cheti cha kughushi
cha tathmini ya uharibifu wa mazingira chenye namba ya usajili
EC/EIA/3366 cha Oktoba 17, 2017 kwa Deogratius Chacha, akijaribu
kuonyesha kuwa cheti hicho ni halali na kimetolewa na Nemc wakati akijua
si kweli.
Katika
shtaka la tano, washtakiwa hao wote wanadaiwa kuwa kati ya Septemba 27
na Aprili 6 ,2018 walijipatia kwa njia ya udanganyifu Sh160 milioni toka
kwa PMM Estate (2001) Ltd kwa madai kuwa wangeweza kufanya tathmini ya
uharibifu wa mazingira na kumpatia cheti ambacho kinatolewa na Nemc
kitendo ambacho si kweli.
Katika
shtaka la sita washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Septemba27, 2016
na Aprili 6, 2018 Dar es Salaam waliisababishia Nemc hasara ya Sh160
milioni.
Baada
ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hao hawakuruhusiwa kuongea
chochote kwa sababu mashtaka ya uhujumu uchumi Mahakama ya Kisutu haina
mamlaka ya kuisikiliza hadi Mahakama Kuu.
Washtakiwa wamepelekwa rumande na kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 14, 2018.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )