AZAM
FC wametoka sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar katika mechi yao
ya 20 msimu wa ligi kuu soka Tanzania bara iliyomalizika jioni hii
uwanja wa Manungu, Turiani, Mkoani Morogoro.
Mabingwa
watetezi Azam walikuwa wa kwanza kuandika bao dakika ya 17' kupitia kwa
nahodha msaidizi, Himid Mao Mkami 'Ninja', lakini dakika tatu baadaye
(dk 20) Musa Hassan Mgosi aliisawazishia Mtibwa Sugar.
Matokeo hayo yanaifanya Azam izidi kuweka reheni ubingwa wake mbele ya vinara Young Africans.
Azam wamefikisha pointi 38' katika nafasi ya pili.
Yanga
wanaendelea kuwa vinara kwa pointi zao 43 baada ya mechi 20, lakini
kesho wanashuka dimbani kuchuana na Mbeya City fc uwanja wa Taifa Dar es
salaam.
Mtibwa Sugar nao wapo katika mazingira magumu na pointi moja ya leo inawafanya wafikishe pointi 24.
Wakata miwa wanahitaji kukwepa kushuka daraja wakati Azam wanahitaji kutetea ubingwa.
Kutokana
na mazingira hayo ilitarajiwa mechi ya ushindani na yenye kashikashi
nyingi, lakini katika dakika zote 90' timu zilicheza mpira wa kawaida.
Kila timu ilitengeneza nafasi, lakini washambuliaji wa timu zote walikuwa butu.
Baada ya mechi ya leo,Azam wanakwenda Tanga kucheza mechi ya kiporo jumatamo ya wiki ijayo.
Mtibwa Sugar wao wanasafiri kwenda Mbeya kuwavaa vibonde wa ligi kuu, Tanzania Prisons jumapili ya wiki ijayo.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )